VIDEO: Kaka wa mwanamke aliyeuawa kisha kuchomwa, asema haikuwa lelemama

Friday July 19 2019

By Elizabeth Edward, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Wiseman Marijani, kaka wa mwanamke aliyeuawa na kuchomwa moto na mumewe, amesema kama wasingesimama imara kufuatilia kutoweka kwa ndugu yao, suala hilo lisingefikia hatua ya sasa.

Pia amesema tabia ya dada yao, Naomi kupenda kila mtu atendewe haki, ndiyo iliyowasukuma kufuatilia kutoweka kwake hadi polisi walipomkamata mumewe kwa tuhuma za kumuua mwenzi wake.

Kamanda wa Polisi wa Temeke, Amon Kakwale alisema juzi kuwa mume huyo, Khamis Luwongo, 38, amekiri kumuua mkewe anayeitwa Naomi, 36, na baadaye kuchimba shimo kwenye banda la kuku ambalo alilitumia kumchoma kwa moto wa magunia mawili ya mkaa na kisha kwenda kufukia majivu shambani.

Kwa mujibu wa polisi, baadaye mumewe alikwenda polisi kutaarifu kuwa Naomi amepotea. Naomi alitoweka nyumbani Mei 15.

Pamoja na polisi kusema mume huyo amekiri kumuua mkewe, familia italazimika kusubiri takriuban siku 10 kuthibitisha kama majivu yaliyopelekwa kufanyiwa kipimo cha vinasaba (DNA) ni ya ndugu yao.

Akizungumza na Mwananchi, Wiseman ameeleza jinsi walivyopata changamoto kufuatilia suala hilo kituo cha polisi hadi lilipohamishiwa Kituo Kikuu cha Dar es Salaam ambako askari walichukua hatua na kumkamata mtuhumiwa.

Advertisement

“Tulifungua jalada la uchunguzi lakini tukaona kimya, ikatulazimu kuanza kufuatilia,” alisema Wiseman.

Alisema baada ya kupata taarifa za kutoweka kwa ndugu yao walizunguka kwenye vituo vya polisi lakini hawakupata matumaini.

Alisema baada ya kutoa taarifa ya kupotea kwa Naomi katika kituo kimoja cha polisi Kigamboni, siku zilikatika bila jalada la uchunguzi kufunguliwa.

“Ninachoweza kusema tungekuwa lelemama hili suala lingekuwa limeisha hivyo. Huenda kupenda kwake haki Naomi ndio kumetufanya leo tufike hapa, alikuwa hakubali kuona mtu ananyimwa haki wala yeye kuonewa.”

“Hilo ndilo lilitusukuma kufuatilia sehemu mbalimbali. Changamoto ikawa ukienda kampuni ya simu ya mtandao aliokuwa anatumia, ilikuwa ngumu kupewa taarifa (za mawasiliano aliyofanya mwishoni) bila barua inayoonyesha kuna jalada la uchunguzi,” alisema.

Alisema kwa takribani siku 17 walizunguka bila kuona mwanga wowote hadi Juni 12 walipofanikisha kuhamishia shauri hilo Kituo cha Polisi Chang’ombe.

Likiwa Chang’ombe, mpelelezi aliandika barua kwa kampuni ya simu kwa ajili ya kupata taarifa za mawasiliano.

“Ninachoweza kusema Mungu alikuwa upande wetu, Ile barua iliandikwa kwa mfumo wa kawaida si kuonyesha kwamba ina haraka. Tulitegemea kwa suala kama hili linalohusisha uhai wa mtu kazi ingefanyika kwa dharura,” alisema.

“Barua ilienda kwa mtindo huo na majibu yalipatikana baada ya wiki mbili. Ile ripoti ilivyotoka mimi ambaye ni mwanafamilia nikawa napitishwa kwenye karatasi kwa kuhojiwa maswali,” alisema.

Alisema pamoja na kupewa ripoti, familia haikulezwa kuwa ingehusikaje kusaidia kutafutwa kwa ndugu yao na hivyo kulazimika kuingilia kati.

“Ukiwa na jambo kubwa kama hili unazungumza na watu mbalimbali nikapata watalaam wakasaidia kuisoma na kuitafsiri ile ripoti ndipo tulipokutana na mambo hayo,” alisema.

“Kilichotuumiza ni kwamba ushahidi ulishakusanywa lakini ilichukua zaidi ya mwezi hatua kuchukuliwa, hadi shauri lilipohamishiwa Central (kituo kikuu cha polisi) ndipo mhusika akakamatwa na hatimaye kukiri,” alisema Wiseman.

Kaka huyo wa marehemu alisisitiza kuwa kwa sasa hawataweka msiba hadi watakapopata taarifa ya polisi kuhusu matokeo ya kipimo cha vinasaba kuthibitisha kwamba mabaki yaliyofukuliwa ni ya Naomi.

“Kwa sasa hatuna tatizo na polisi, tumeliacha suala hili mikononi mwao na tuna imani huu ni mwanzo,” alisema.

“Mategemeo yetu uchunguzi zaidi utafanyika ili kumbaini kila aliyehusika katika suala hili.”

Advertisement