Kakobe: Nilifahamu kauli ya Gwajima itakuja na majibu

Muktasari:

Askofu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe amesema neno alilolitoa Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima katika sherehe za kanisa lake kutimiza miaka 30 alijua litakuwa na majibu

Dar es Salaam. Askofu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe amesema neno alilolitoa Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima katika sherehe za kanisa lake kutimiza miaka 30 alijua litakuwa na majibu.

Akizungumza katika mahubiri katika Kanisa la Ufufuo na Uzima leo Jumapili Mei 12, Kakobe amesema sherehe hizo zilihudhuriwa na manabii na wachungaji kutoka makanisa mbalimbali, huku mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda naye akialikwa.

Ametoa kauli hiyo huku akirejea picha ya video inayosambaa mitandaoni ikimuonyesha mtu aanayedaiwa kuwa ni Askofu Gwajima akiwa faragha na mwanamke ambaye hajafahamika, akisema wapo wataalam wa kutengeneza video za uongo.

Kakobe amesema wengi walichukia kwa nini Makonda alialikwa katika sherehe hizo na wengine walichukia zaidi baada ya Gwajima kukumbatiana na mkuu huyo wa mkoa huku wakibaki kutega masikio leo wakisubiri kuanzisha awamu ya pili ya mafarakano jambo ambalo halipo.

“Kwa neno alilolitoa Gwajima lilikuwa limejaa upako nilijua tu kuna kitu lazima kitokee na kama isingekuwa hivyo basi shetani angekuwa amekufa,” amesema Kakobe.

Amesema shetani hapendi kuona watu wakiwa wamoja na ndiyo maana hujaribu kuwatawanya ili iwe rahisi kuwatawala.

“Mshikamano huu wa wachungaji na manabii shetani wa kuubomoa bado hajazaliwa kwa sababu shetani anajua mkiwa wamoja katika kristo, baraka za Mungu ndiyo zinapowajia,” amesema Kakobe.