Kakobe: Ninaamini Gwajima umewasamehe waliokukosea

Sunday May 12 2019

By Aurea Simtowe, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Askofu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe amesema ana amini Askofu wa Kanisa la Ufufo na Uzima, Josephat Gwajima amewasamehe  waliomkosea kwa maelezo kuwa kufanya hivyo ni moja kati ya vigezo vya ukomavu katika imani.

Amesema hayo leo Jumapili Mei 12 katika kanisa la Ufufuo na Uzima linaloongozwa na Askofu Gwajima lililopo Ubungo Dar es Salaam katika mahubiri katika ibada ya Jumapili, huku akigusia picha ya video zinazomuonyesha mtu mwenye sura inayofanana na ya Gwajima akiwa faragha na mwanamke ambaye bado hajafahamika.

Amesema hata maandiko yanasema bila kusamehe hata sadaka yako haiwezi kupokelewa hivyo aliwataka waumini kuendelea kumtia moyo ili aendelee kuwa na moyo wa msamaha.

“Msamaha kwetu wa Kristo ni sehemu ya maisha yetu, bila kusamehe hata sisi wenyewe hatuwezi kusamehewa, tumewasamehe wote waliotukosea na tumtie moyo aendelee kuwa na roho ya msamaha tena bila masharti. Hata kwa mwanasiasa kusamehe na kusahau ni moja ya vigezo vya ukomavu wa kisiasa,” amesema Kakobe.

Amesema amefurahi kushiriki ibada katika kanisa hilo kwa sababu alikuwa akisikia majeshi ila leo amethibitisha kuwa kanisa hilo ni jeshi la Mungu.

“Kwa hiyo mnanitengenezea video na mimi nawaambia katika miaka 30 ya huduma hii nimekwepa mishale mingi sana, kanisa la Mungu Tanzania limejengwa juu ya miamba hakuna mtu anaweza kulitikisa.”

Advertisement

“Nimeacha ibada yangu kule sasa hivi nairudia, mtumishi wa Mungu (Gwajima) nikuachie madhabahu usizungumzie habari hizi shughuli tumeshaimaliza,” amesema Kakobe.

Advertisement