Kakobe: Sikubali mashtaka ya Gwajima, tutaendelea kushirikiana na Makonda

Sunday May 12 2019

 

By Aurea Simtowe, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Askofu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe amesema anakataa mashtaka ya Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima huku akiwataka waumini wa kanisa hilo kuyakataa.

Amesema kabla ya mtu hajapandishwa juu ni lazima ashushwe chini huku akiwahakikishia waumini kuwa kuna utukufu mkubwa unakuja mbele yao.

Kakobe ametoa kauli hiyo leo Jumapili Mei 12 katika mahubiri yake kwenye kanisa la Ufufuo na Uzima linaloongozwa na Gwajima, wakati akizungumzia picha za video zilizosambaa mitandaoni zikimuonyesha mtu aliyefanana na Gwajima akiwa faragha na mwanamke ambaye hajatambulika.

“Moja kati ya sifa ambazo Mungu anazitafuta kwa mtumishi wa Mungu ni ujasiri, Gwajima ni jasiri kama simba na naona fahari kuwa na mtumishi kama huyu, mama una mume jasiri.”

“Ninajivunia kuwa na wewe. Ninaona fahari kuwa juu ya Askofu Gwajima na ninaona fahari kwenu waumini nyote na huu ni wakati wa kumthibitishia shetani kuwa kanisa hili limejengwa juu ya mwamba na ninaomba ibada zote zinazofuata kila mmoja awepo ili mthibitishe kuwa kanisa hili limejengwa juu ya imani,” amesema Kakobe.

Amesema kutokana na suala lililotokea watu walitarajia kuona makanisa mengi yakimtenga Gwajima ila hilo ni tofauti kwa sababu yeye amempenda sana hivi kuliko zamani.

Advertisement

“Mwenye wivu ajinyonge lakini huyu nimempenda sasa kuliko wakati wowote uliopita, hawa mabingwa wa fitina  walijaribu kupeleka hadi kwa Makonda  (Paul- Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam) ambaye alijaribu kuamini lakini alishtuka.”

“Tulimleta Makonda kwa sababu sisi ni wazee wa taifa, kama Makonda ana upungufu tunamsaidia sasa tukimtenga tutamsaidiaje tutaendelea kushirikiana naye, tunawapenda watu wote,” amesema Kakobe.

Advertisement