Kakunda awajibu Nape, Selasini

Muktasari:

Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda amesema ataunga mkono kufanyika kwa uchunguzi wa ununuzi wa korosho ikiwa utajikita katika upatikanaji wa malighafi za kutosha viwandani na wakulima kulipwa vizuri

Dodoma. Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda amesema ataunga mkono kufanyika kwa uchunguzi wa ununuzi wa korosho ikiwa utajikita katika upatikanaji wa malighafi za kutosha viwandani na wakulima kulipwa vizuri.

Kakunda ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Mei 20, 2019 bungeni jijini Dodoma akijibu hoja za wabunge, Joseph Selasini (Rombo) na Nape Nnauye wa Mtama ambao katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Kilimo mwaka 2019/2020 walipendekeza kamati itakayoundwa na Bunge au Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kukagua ununuaji wa korosho.

Kakunda amesema  unahitajika uchambuzi wa kina utakaofanywa na Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi ili kuweka mfumo wa kuhakikisha viwanda vinapata malighafi ya kutosha.

“Ushindani wa bei umekuwa mkubwa kiasi kwamba viwanda vyetu vinapata shida kushindana na kampuni nyingine,” amesema Kakunda.

Amebainisha kuwa katika miaka 10 viwanda vingi vya korosho nchini vimekufa kwa sababu ya ushindani ulipo katika soko.

Kuhusu baadhi ya wabunge kutaka viongozi kuwajibika  kwa mashtaka kwa uhujumu, Kakunda amesema uhujumu uchumi ni suala la kisheria ambalo lina utaratibu wake ikiwemo kukamilisha uchunguzi wa kutosha dhidi ya mashtaka husika kabla ya kuyafungua.

“Wakati tunamwachia Mwanasheria mkuu wa Serikali katika jambo hilo tunatambua kabla ya Rais hajachukua hatua ya kumkomboa mkulima kwa kumlipa Sh3,300 kwa kila kilo (ya korosho) hakuna kampuni hata moja ambayo ilikuwa imefikia ofa hiyo,” amesema Kakunda.

Amesema baada ya  Serikali kutamka kununua korosho zilijitokeza kampuni na kusema zinaweza kulipa kwa bei hiyo au zaidi.

Amesema kama wabunge wanataka uchunguzi uelekee katika kupata malighafi ya kutosha na mkulima alipwe vizuri, atawaunga mkono.