Kalemani, Kamati ya Bunge wazungumzia mradi wa umeme Rufiji

Mratibu wa mradi wa uzalishaji Umeme wa Rufiji wa shirika la umeme Tanzania Tanesco Justus Mtolera (mwenye shati la maua) akieleza juu ya mradi huo  anavyoendelea wajumbe wa kamati ya bunge ya Nishati na Madini, waliotembelea mradi huo,kulia ni  Waziri wa Nishati Dk Medard Kalemani na Mwenyekiti wa kamati hiyo Dastan Kitandula.

Muktasari:

  • Waziri wa Nishati Dk Medard Kalemani ameihakikishia Kamati ya Bunge ya Nishati kuwa mradi wa umeme utakapokamilika utakuwa na manufaa kwa Watanzania.

Rufiji. Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani amewahakikishia wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kuwa kukamilika kwa mradi wa kufufua umeme katika Mto Rufiji utakuwa na faida kwa Taifa pamoja na Watanzania kupata ajira hususani vijana.

Dk Kalemani amesema hayo leo Ijumaa Machi 15, 2019 baada ya kamati hiyo ya Bunge kutembelea eneo la mradi wa umeme na kujionea kazi mbalimbali zikiwemo zilizokamilika na zinazoendelea.

Maeneo waliyotembelea ni barabara, miundombinu ya reli, madaraja ambayo tayari yamemalizika kujengwa na eneo ambako litajengwa bwawa kubwa la maji.

Amesema ajira 3,000 hadi 5,000 zitapatikana wakati na baada ya ujenzi wa mradi huo, na baada ya kukamilika kwake ajira za kudumu zitakuwa 250 hadi 400 na kwamba hayo ni manufaa kwa nchi.

Aidha amesema kukamilika kwa mradi huo kutanufaisha wananchi katika shughuli za uvuvi na kilimo cha umwagiliaji kwa sababu ya kujengwa kwa bwawa kubwa lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita za ujazo 35.2 bilioni.

Mwenyekti wa kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, Dastan Kitandula amesema kamati yao imeridhishwa na namna ujenzi huo unavyoendelea na kwamba katika tasnia ya nishati ya umeme, wa maji pekee ndio wa bei rahisi hivyo ni vyema Watanzania wakategemea manufaa ikiwamo kuinua uchumi wa nchi.

Kitandula amewataka wafanyabiashara kutumia fursa ya kuwepo kwa mradi huo kwa kuhakikisha wanapata tenda zinazotokea katika ujenzi wa mradi huo.