Kalemani awatega Tanesco Kigoma

Waziri wa Nishati, Medard Kalemani

Muktasari:

  • Serikali imemtaka meneja wa Tanesco wilayani Kakonko kujiuzulu endapo wananchi wa wilaya hiyo hawatapata umeme kufikia Juni 30 mwaka huu.

Kakonko. Waziri wa Nishati, Medard Kalemani amemtaka Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma, Enock Bwire, kuandika barua ya kujiuzulu ikiwa watashindwa kusimamia usambazaji wa umeme kupitia Mradi wa Umeme Vijijini (Rea) ifikapo June 30, 2019.

Akizungumza leo Jumapili Machi 24, 2019 na wananchi wa kata ya Kasanda wilayani hapa mkoani Kigoma, Kalemani amesema ifikapo tarehe hiyo vijiji vyote 29 vya wilaya hiyo umeme uwake kila nyumba hata kama ni ya nyasi.

Waziri Kalemani amemsisitizia mkandarasi wa mradi huo, Teddy Nyagawa, kukatwa asilimia 10 ya mshahara wake endapo hawataenda na kasi hiyo, kwa lengo la kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa na umeme katika maeneo yao.

"Viongozi wote wa Tanesco ni marufuku kukaa ofisini, kila mmoja aende kuhudumia wananchi, kazi yetu ni kuwahudumia wao," amesema Waziri Kalemani.

Amesema lengo la kufika mkoani Kigoma ni kumsukuma mkandarasi kufanya kazi kwa kasi ya juu huku akimtaka kuchukua vibarua ndani ya maeneo hayo na si kuchukua nje ya hapo kwa lengo la kumaliza mapema mradi huo.

Waziri Kalemani amemtaka mkandarasi wa mradi huo kuhakikisha wanawasha umeme katika vijiji vitatu kwa wiki kwa wilaya hiyo na kwa awamu ya kwanza vijiji 149 vya awali vitapata umeme mkoani hapa.