Kamati ya Bunge yabaini kasoro uagizaji sukari nje ya nchi

Muktasari:

Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira imeshauri Serikali kabla ya kutoa vibali kwa mwaka 2019 ifanye tathimini upya kwa lengo la kubaini uwezo wa viwanda na upungufu (gap) la sukari .

Dodoma. Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira imekosoa utaratibu wa utoaji wa vibali vya kuingiza sukari ambapo imesema vimekuwa vikitolewa bila kuzingatia upungufu wa sukari iliyopo kwa wakati husika.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Suleiman Saddiq ameyasema hayo leo Jumatatu Februari 4 2019, wakati akiwasilisha taarifa ya shughuli za kamati hiyo kwa kipindi cha kuanzia Machi, 2018 hadi Januari, 2019 kwa Bunge.

Amesema jambo hilo linatoa mianya kwa wafanyabiashara wasio waaminifu kuamua kupunguza uzalishaji na kuingiza sukari zaidi ya kutoka nje ya nchi.

“Kwa kuwa hatua ya kupunguza uzalishaji ina madhara katika ajira, Bunge linaishauri Serikali kabla ya kutoa vibali kwa mwaka 2019 ifanye tathimini upya kwa lengo la kubaini uwezo wa viwanda ndani na upungufu (gap) la sukari,” amesema.

Amesema hatua hiyo itasaidia kubaini mahitaji halisi lakini pia kujua sifa za waombaji na kuondoa hali ya sintofahamu inayoendelea sasa.