Kamati ya Bunge yaishauri WHC kuwa wabunifu

Muktasari:

 

 

  • Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) leo imefanya ziara miradi ya ujenzi wa makazi eneo la Gezaulole na Bunju B jijini Dar es Salaam

Dar es salaam.  Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeshauri ubunifu zaidi katika nyumba zinazojengwa na Watumishi Housing Company (WHC) ili kuimarisha ushindani.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Naghenjwa Kaboyoka, amesema lengo lake  ni kuhakikisha fedha za umma zinazowekezwa katika miradi hiyo zinarejeshwa bila hasara.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano Machi 20, 2019 wakati wa ziara ya miradi ya ujenzi wa makazi ya Gezaulole uliopo Kigamboni na Bunju B, jijini Dar es salaam. 

"Inabidi kuongeza ubunifu ili isionekane kuwa ni nyumba za watumishi pekee, wanatakiwa kushawishi mazingira ya upatikanaji huduma za afya, shule na viwanja vya michezo, maegesho ya magari katika uzio wa nyumba," amesema Kaboyoka.

Naye mtendaji mkuu wa kampuni hiyo Dk Fred Msemwa, amekubaliana na ushauri huo akisema tayari eka 2.5 kwenye mradi wa Bunju B zitatumika kujenga zahanati, shule na viwanja vya michezo.

Dk Msemwa amesema katika utekelezaji wa miradi hiyo, tayari wamekamilisha asilimia 98 ya nyumba 329 katika awamu ya kwanza ya mradi wa Gezaulole huku asilimia 50 zikiwa zimeshanunuliwa.

Amesema kampuni hiyo inayojenga na kukopesha nyumba kwa malipo ya ukomo wa miaka 25, itajenga jumla ya nyumba 795 katika mradi wa Gezaulole.

Kwa mujibu wa taarifa ya WHC, tayari Sh19.53 bilioni zimetumika kati ya Sh21.77 bilioni za mradi huo. Gharama ya kuuza nyumba hizo ni kati ya Sh49 milioni hadi Sh96 milioni.

Pia, amesema kuhusu mradi wa Bunju B ujenzi umekamilika kwa asilimia 98 ya nyumba 64 zinazojengwa hapo, huku zaidi ya nyumba 20 zikiwa zimeshanunuliwa.