Kamati ya Bunge yataka ofisi, taasisi za Serikali kutumia huduma za TTCL

Muktasari:

 

  • Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) leo Jumatano imetembelea miradi inayotekelezwa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) na kutoa wito kwa taasisi na ofisi za Serikali kutumia huduma zinazotolewa na shirika hilo.

Dar es Salaam. Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imezitaka taasisi, ofisi na maofisa wa Serikali kuongeza matumizi kwenye huduma zinazotolewa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL).

Mwenyekiti wa kamati hiyo Dk Raphael Chegeni, amesema hayo leo Jumatano Machi 20, 2019 baada ya kuitembelea miradi inayosimamiwa na shirika hilo na kushuhudia uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali na kubaini changamoto kubwa ni matumizi.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea miradi hiyo, Dk Chegeni amesema kuongezeka kwa matumizi ya huduma hasa kwa ofisi na taasisi za Serikali kutachangia utendaji wa kibiashara wa shirika hilo.

“Matumizi yanayofanywa sasa hivi yapo chini ya kiwango. Ni muhimu kuongeza matumizi katika hizi huduma kama za kimtandao na data, ukizingatia Serikali imewekeza fedha nyingi sana katika miradi ya mawasiliano hasa kwenye shirika hili,” amesema.

Katika kusisitiza matumizi ya huduma za shirika, mwenyekiti huyo amesema kiwango cha matumizi kinavyoongezeka kitasababisha kukuza faida kwa shirika na ukuaji wa gawio kwa Serikali.

Katika kutembelea miradi iliyo chini ya TTCL, kamati ya ilipata nafasi ya kuutembelea mkongo wa taifa pamoja na kituo cha kutunzia taarifa (Data center) kilicho chini ya shirika.

“Tumeona jinsi mkongo wa taifa unavyofanya kazi, unavyochangia katika kulinda usalama wa nchi  na kuchochea maendeleo kupitia sekta ya mawasiliano,” amesema Dk Chegeni.

Naye mwenyekiti wa bodi ya TTCL Omari Nundu, amesema shirika limekuwa likijizatiti kuhakikisha linaleta matokeo chanya ya biashara  kwa kubuni bidhaa mpya na kuongeza upatikanaji mtandao wake sehemu mbalimbali nchini.

Nundu alisema kwa sasa shirika limefanikiwa kwani wameweza kuongeza wateja kwenye soko kutoka asilimia 0.85 na kufikia asilimia 2. Na upatikanaji mtandao umepanuka zaidi hasa mikoani.

“Kutoka kwenye kampuni inayotengeneza hasara mpaka kuwa shirika linalopata faida. Mwaka jana tulitoa Sh1.5 bilioni kama gawio kwa Serikali,” amesema.