Kamati yataka watumishi EAC wachukuliwe hatua za kinidhamu

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Dk Damas Ndumbaro akisoma hotuba ya makadirio ya bajeti ya mwaka wa fedha 2019/2020 jijini Arusha leo.Picha na Filbert Rweyemamu

Muktasari:

Kamati ya Bunge la Hesabu la Afrika Mashariki(Eala) imelitaka Bunge hilo kulielekeza baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuwachukulia hatua watumishi wa jumuiya hiyo waliobainika kukiuka kanuni na miongozo ya manunuzi na ajira.


Arusha. Mvutano mkali wa hoja umeibuka wakati wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala) wakijadili taarifa ya Kamati ya Hesabu ya hesabu zilizokaguliwa za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 30,2017.

Taarifa hiyo ambayo ilishasomwa katika  moja ya vikao vilivyopita, wabunge waliikataa kwakua ilieleza upungufu mbalimbali wa ukiukwaji wa taratibu za kifedha, ajira za muda na sheria za manunuzi lakini haikutaja majina ya maofisa waliosababisha hasara na hatua ambazo kamati inapendeza zichukuliwe.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk Ngwaru Maghembe alisema wakati wakipitia taarifa ya Kamisheni ya Ukaguzi wa EAC, mihimili yake na taasisi ambazo zipo chini yake katika mwaka huo wa fedha Jumuiya ilikua na bajeti ya dola 106,494,898 wakati matumizi yalikua dola 66,358,844 bajeti ikiwa imetekelezwa kwa asilimia 62.

Alisema katika mwaka huo wa fedha ulioishia Juni 30,2017 michango ya wahisani ilikua imepungua sana na kuathiri kwa kiwango kikubwa mipango na shughuli za taasisi za EAC na kwamba kutokana na upungufu wa fedha unaozikabili taasisi za EAC ni muhimu kuweka malengo yanayotekelezeka.

“Mchakato wa manunuzi kwenye mihimili ya EAC na taasisi zake ulikua unakiuka taratibu za manunuzi, kutokufuata taratibu za mikataba ya  ajira pamoja na utoaji wa ajira za muda mfupi ni mambo yanayokiuka kanuni na taratibu za ajira na mkataba ulioanzisha  EAC,” alisema Dk Maghembe

Katika taarifa yenye kurasa 164, Dk Maghembe alisema EAC iliendelea kupitia kipindi kigumu cha kifedha kutokana na taasisi zake kutokupata unafuu wa kodi ya ongezeko la thamani VAT katika nchi wanachama zilizo taasisi hizo, wakati fedha hizo zingeweza kusaidia utekelezaji wa miradi ya jumuiya.

Eneo jingine ni kuchelewa utekelezaji wa mapitio ya kitaasisi ambayo yalikubaliwa zaidi ya miaka 10 iliyopita lakini utekelezaji wake hadi sasa haujafanyika ukiwa umekwama katika ngazi ya baraza la Mawaziri wa EAC.

Kabla ya kusomwa kwa taarifa hiyo kulikua na mvutano wa wabunge ambao walitaka majina ya maofisa wa Sekretarieti waliosababisha hasara na kutotimiza wajibu wao ipasavyo watajwe majina huku baadhi yao wakipinga kuwa wasitajwe na Spika wa Bunge hilo, Martin Ngoga kuwahoji na waliotaka watajwe walishinda.

Alisema kamati yake  ilikabidhiwa hesabu zilizokaguliwa za mihimili na taasisi 16 na kisha kuzipitia na kubaini  mambo kadhaa kwaajili ya kuyatolea mapendekezo  na matokeo ya ukaguzi wa taarifa za fedha  kwenye Sekretarieti ya EAC, miradi na programu mbalimbali katika mwaka ulioishia Juni 30,2017.

Pia matokeo ya ukaguzi  wa taarifa za fedha mihimili ya EAC na taasisi zake pamoja na mtazamo wao na mapendekezo hayo.

Hata hivyo, taarifa hiyo imewataja baadhi ya maofisa waandamizi kati yao wameshamaliza mikataba yao ya ajira kushindwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo kwa kutokufuata ipasavyo kanuni na miongozo iliyowekwa.

Mwenyekiti wa wabunge wa Tanzania katika Bunge hilo, Dk Abdullah Makame alisema ni wakati muafaka kwa watumishi wa taasisi zote za EAC kutambua umuhimu wa matumizi sahihi ya fedha za umma na kufuata miongozo iliyopo.