Kampuni China yatangaza neema kwa wakulima Tanzania

Muktasari:

Ubalozi wa Tanzania Beijing, China umebainisha kuwa kampuni moja nchini China imewasilisha ombi la kununua ufuta, karanga na maharage ya soya kutoka Tanzania


Dar es Salaam. Ubalozi wa Tanzania Beijing, China umebainisha kuwa kampuni moja nchini China imewasilisha ombi la kununua ufuta, karanga na maharage ya soya kutoka Tanzania.

Taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Desemba 20, 2018 na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tan Trade) na kusainiwa na mkuu wa kitengo cha mawasiliano wa mamlaka hiyo, Theresa Chilambo inaeleza kuwa kampuni hiyo inalenga kununua bidhaa hizo kwa vigezo.

Kampuni hiyo inahitaji ufuta tani 3,000 kwa mwezi, karanga tani 2,000 kwa mwezi na maharage ya soya tani 5,000 kwa mwezi

Akizungumza na Mwananchi leo,  Theresa amesema ufuta unaotakiwa ni wa ubora wa Taifa daraja la pili.

Amebainisha kuwa hata karanga na maharage ya soya yanayohitaji  nayo ni katika kiwango hicho cha ubora.