Kampuni sita zasaini mkataba wa awali kununua korosho nchini Tanzania

Thursday May 16 2019

Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda

Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo. Picha na Ericky Boniphace 

By Sharon Sauwa, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Serikali imesaini mkataba wa awali na kampuni sita ya kununua korosho kati ya zilizoomba kununua korosho hizo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Mei 16, 2019 Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda amesema baada ya Kampuni ya Indo Power ya nchini Kenya kushindwa kununua korosho wameendelea kusaini mikataba ya awali.

“Tumeendelea kusaini mikataba ya awali na kampuni nyingine hadi sasa tumesaini na kampuni sita,” amesema.

Amesema asingependa kuzitaja kampuni hizo kwa sababu ya hali halisi ya biashara ya korosho duniani ambayo kwa sasa watu wanafuatiliana na kuharibiana biashara.

Kakunda amesema Novemba 13 mwaka jana hadi juzi,  Serikali imenunua tani 225,000 za korosho na kwamba kati ya hizo 2,200 zinaendelea kubanguliwa na viwanda vya ndani kwa mkataba maalumu.

Amesema tani 222,800 za korosho zimebaika katika maghala na zina ubora wake.

Advertisement