Kampuni ya A. Kusini kununua hisa Voda kwa Sh499 bilioni

Friday August 9 2019

 

By Ephrahim Bahemu na Alawi Masare [email protected]

Dar es Salaam. Mamlaka za usimamizi nchini zimetoa vibali vyote muhimu kwa ajili ya mauzo ya hisa za kampuni ya huduma za simu ya Vodacom Tanzania, hatua ambayo itaifanya kampuni mama ya Vodacom Group kuweza kumiliki hadi asilimia 75.

Novemba mwaka jana wanahisa wa Vodacom Tanzania waliidhinisha kuuzwa kwa asilimia 26.25 ya hisa zake kwa kampuni ya Vodacom Group zilizokuwa zikimilikiwa na kampuni ya Mirambo Limited.

Vodacom Group ya Afrika Kusini, ambayo kwa sasa inamiliki asilimia 61.6 ya hisa za Vodacom Tanzania, itaongeza umiliki wake baada ya kununua hisa milioni 588 za Mirambo Limited kwa gharama ya Sh499.8 bilioni.

Mirambo itapata Sh850 kwa kila hisa moja ambayo ni kubwa kuliko bei ya sasa ambayo ni Sh800 kwa hisa moja. Bei inayotolewa na Mirambo kwa Vodacom Group ni sawa na ile ya mauzo ya awali kwa umma (IPO).

Kwa mujibu wa taarifa ya Vodacom Group ambayo imeorodheshwa katika soko la hisa la Johannesburg, idhini ya maombi ya muamala huo imetolewa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA), Tume ya Ushindani (FCC) na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

“Muamala utafanyika katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) kama mauzo ya moja kwa moja (Pre-arranged transaction),” inaeleza taarifa hiyo.

Advertisement

Utaratibu wa mauzo ya moja kwa moja ambao unaruhusiwa ndani ya DSE, unatoa mwanya kwa muuzaji na mnunuzi kupanga bei kabla ya tangazo la kuuza hisa hizo.

Vodacom Group imesema tayari imeandaa taratibu zote za malipo kupitia benki moja ya kibiashara ya nchini ambayo haikutajwa katika taarifa hiyo.

“Malipo ya hisa hizo yatatokana na vyanzo mbalimbali vya fedha vikiwemo vya ndani, akiba ya kampuni, na mkopo. Kuna uhakika wa fedha za kufanya hivyo,” inasema taarifa hiyo.

Madalali wa DSE walisema kukamilika kwa manunuzi ya hisa hizo kutakuwa na matokeo chanya kwa kuwa watu watakuwa na imani nazo hivyo wawekezaji wanaweza kuchagua kubaki na hisa zao au kuongeza nyingine zaidi.

“Wakati mwekezaji mkubwa anapoongeza hisa zake, humaanisha kuna thamani ambayo pengine kwa wengine haijaonekana,” anasema Raphael Masumbuko, mtendaji mkuu wa kampuni ya udalali ya Zan Securities.

“Anakuwa na imani kuwa yajayo katika kampuni hiyo ni ya manufaa. Hatua hii bila shaka itaongeza bei.”

Dalali mwingine ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini alisema kampuni ya Vodacom Group ina imani na ukuaji wa kampuni yake tanzu na pengine inajaribu kutimiza matakwa ya kisheria katika suala la umiliki.

Hivi sasa Serikali inataka kampuni zote za mawasiliano ya simu kuorodhesha walau asilimia 25 ya hisa katika soko la hisa.

Mpaka sasa Vodacom Tanzania, ambayo ina wateja zaidi ya milioni 14.2, ndiyo ambayo imeshatekeleza takwa hilo la kisheria. Iliweka hisa zake sokoni Agosti 2017.

Mwaka juzi, Vodacom Tanzania iliweka sokoni hisa za thamani ya dola 213 milioni za Kimarekani (sawa na zaidi ya Sh430 bilioni za Kitanzania) kwa ajili ya kununuliwa na umma, kiwango ambacho ni kikubwa kuliko vyote Tanzania.

Advertisement