Kampuni ya Marekani yalizwa Sh1.24 bilioni ununuzi wa korosho Tanzania

Muktasari:

Kampuni ya KLM Capital ya Marekani inayowekeza kwenye mazao ya kilimo nchini, inadai kutapeliwa mtaji wa Sh1.24 bilioni ilizotoa kwa kampuni ya Eagle Investment and Logistics (T) Ltd kwa ajili ya ununuzi wa korosho kwa msimu wa 2017/18.


Dar es Salaam. Kampuni ya KLM Capital ya Marekani inayowekeza kwenye mazao ya kilimo nchini, inadai kutapeliwa mtaji wa Sh1.24 bilioni ilizotoa kwa kampuni ya Eagle Investment and Logistics (T) Ltd kwa ajili ya ununuzi wa korosho kwa msimu wa 2017/18.

Madai hayo yameripotiwa Polisi kupitia (RB) CD/IR/2270/2018 ikitaja kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, huku mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai, Kamishna Robert Boaz akikiri kuifahamu kesi hiyo alipoulizwa na Mwananchi kwa simu.

“Hiyo kesi naijua inapelelezwa hapo kwa ZCO (Ofisa Upelelezi wa Kanda) na najua jalada lipo kwa mwanasheria wa Serikali kwa ajili ya kuandaliwa mashitaka,” alisema Kamishna Boaz.

Mkurugenzi wa Eagle Investment and Logistics (T) Ltd, Migisha Alabasha Hume amezungumza na Mwananchi kwa simu na kukiri kuwepo kwa madai hayo Polisi, lakini hakutaka kuingia kwa undani.

“Ni kweli nafahamu, ila hayo mambo yako Polisi, siwezi kuyazungumzia. Uchunguzi unafanyika, wakikamilisha mtaambiwa,” alisema Hume.

Jinsi fedha ‘zilivyopigwa’

Mmoja wa wamiliki wa kampuni hiyo ya Kimarekani ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema alianza kufanya biashara na Hume tangu Septemba 2017 kwa kuwa alikuwa akimfahamu kwa muda mrefu. “Nilianza biashara na Migisha Hume, kwa sababu yeye na familia yangu ni marafiki sana. Kabla ya kuingia kwenye biashara hiyo nilizungumza na mama yake na kaka yake nikawauliza kama ndugu yao anaweza kufanya hii kazi,” alianza kusimulia Mmarekani huyo mwenye asili ya Tanzania.

Mmarekani huyo anayeishi Boston alisema walifahamiana na Hume wakiwa wote nchini humo, lakini baadaye (Hume) aliondoka na kwenda masomoni nchini India kabla ya kurudi Tanzania mwaka 2014 akiwa anafanya biashara.

“Kuna wakati aliwasiliana na mimi akisema kuna biashara ya korosho anayoifanya ila amepungukiwa mtaji. Akasema anahitaji Dola 50,000 kwa ajili ya kununua ‘bid security’ ya kufanya hiyo biashara,” alisema.

Aliendelea kusimulia kuwa Hume alimweleza kuwa kuna kampuni ya Vietnam inamtaka awe na ‘bid security’ halafu itanunua kwake korosho kisha kampuni hiyo ndiyo italipa. “Mimi nikaona ni sawa kwa sababu mwisho wake commission (udalali) inalipwa na tunagawana. Basi nikaenda nimkampa hiyo hela,” alisema.

Hata hivyo, anasimulia kuwa Hume alimwambia walipokwenda Bodi ya Korosho (CBT) kuweka zabuni ya kununua korosho ikaonekana bei imekuwa juu, huku kampuni ya Vietnam ikitaka kuongeza mzigo ufike tani 1000.

“Kwa hiyo akasema nimwongeze hela, nikamwambia ni sawa haina shida. Hayo malipo yote tuliandikishana mkataba ambao nilimtumia akausaini na mwanasheria wake na kunirudishia,” alisema.

Baada ya kutoa fedha hizo, alisema Hume alimhakikishia kuwa wameshanunua korosho. Hata hivyo ilichukua muda mrefu kurejesha fedha hizo.

“Nikawa namfuatilia, namwuliza vipi, mbona hatulipwi? Baada ya miezi sita tangu Septemba 2017 ndiyo akasema tumelipwa. Nikasema kama tumeshalipwa nionyeshe kwenye akaunti nione. Akanitumia ‘statement’ ya akaunti yake ikionyesha kuna fedha zimeingia.

Alisema licha ya kuonyeshwa taarifa ya malipo ya benki ya NMB tawi la Mlimani City, aliwapigia simu ili kuhakikisha kama ni kweli fedha zimetumwa.

“Niliambiwa kuna mtu katika benki hiyo ndiyo aliyetuma fedha. Nikauliza huyo mtu anafanya kazi hapo? Wakanijibu kuwa yupo. Nikaomba kuzungumza naye nikamwuliza, huyu mtu (Migisha) huu mwamala wake ni wakweli? Kuna risiti?

“Akajibu ndiyo lakini itabidi umwulize zaidi taarifa zake, mimi siwezi kukutumia. Basi nikaridhika nilipoona ni halisi,” alisema.

Baada ya kujiridhisha, Mmarekani huyo anasimulia kuwa Hume aliwasiliana naye akisema amepata mteja mwingine ili waendeleze biashara.

“Nikamjibu sawa kwa sababu tayari tuna ‘bid security’ na fedha ya kununua mzigo tuendelee, lakini nilimwambia kwa kuwa hii biashara sasa imekuwa kubwa inabidi mimi sasa nije Tanzania nisimamie, ila uwe wazi kwangu nione kila kinachofanyika,” alisema huku akiongeza kuwa aliwatumia mawakili wake kusaini mikataba na Hume.

Alisema alilazimika kuja Tanzania baada ya kuona ‘biashara imekua’ na alipofika akamwongeza Hume kiasi kingine cha fedha.

“Tulikutana mara nyingi hapa Dar es Salaam na nikamtumia fedha kwenye akaunti yake. Akasema kuna kampuni yenye jina la RAJ Dry Fruits ameingia nayo mkataba na wahusika watakuja kuchukua mzigo na atawapa hundi,” alisema.

Anasema alipotaka kuziona korosho zenyewe, Hume alimpeleka Masasi ambako alimwonyesha maghala yaliyokuwa yamejaa magunia ya korosho alizodai kuwa zilikuwa nao.

Aliongeza; “Sikuwa na wasiwasi kwa kuwa niliweza kuangalia akaunti yake na kujua fedha iliyoingia. Kumbe walipokuja akasaini cheki, alichowapatia sivyo mambo yalivyokwenda.”

Anasema alishangazwa na kuchelewehwa kwa malipo ya biashara hiyo na kumshauri Hume watafute mteja mwingine.

“Yeye alikataa akisema hao RAJ tayari wameshalipa malipo ya awali (down payments) ambayo ni asilimia 25. Nikasema ni sawa kwa sababu sisi hatutatoa hela nyingi,” alisema. Hata hivyo anasema ilipofika Mei 2018 ambao ndiyo ulikuwa mwezi wa mwisho wa kuuza mzigo wao kwa mujibu wa mkataba, alishauri tena watafute mteja mwingine, jambo ambalo alisema halikufanyika ilipofika Julai 2018.

“Kwa kuwa muda ulikuwa umekwenda nikaanza kufuatilia upya. Kwa sababu alinipeleka Masasi kuangalia korosho, lakini alisema kuna mzigo mwingine Liwale (Lindi).

“Basi nikamtuma mjomba wangu akahakikishe tena na alipokwenda akaniambia hakuna mzigo wowote.”

Miongoni mwa vielelezo ambavyo Mwananchi imeviona ni hundi ya benki ya KCB Na.000007 iliyotolewa Februari 16, 2018 na kampuni ya Eagle Investment and Logistic TZ Ltd ikilipa Dola 198,000 kwa chama cha ushirika cha Liwale.

Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na Mwananchi umebaini kutokuwepo kwa chama hicho. Akizungumza kwa simu na mwandishi wa habari hizi, mwenyekiti wa Chama cha Ushirika cha Likongowele wilayani Liwale, Sikudhani Mbega alisema vyama vilivyopo wilayani humo mbali ya chama hicho ni pamoja na Umoja, Mshikamano na Tumiliki.

“Hakuna chama cha ushirika Liwale na wala hatujawahi kufanya biashara na hiyo kampuni,” alisema Mbega.

Alisema mjomba wake pia alikwenda Bodi ya Korosho Tanzania kuulizia kama kampuni ya RAJ Dry Fruits na Eagle Investment and Logistics (T) Ltd ilinunua korosho, wakasema wameangalia kumbukumbu zao za miaka miwili hawaoni kampuni hiyo kununua korosho.

Alisema hata baada ya kuonyesha risiti ambazo Hume alidai ni za Bodi ya Korosho, hazikuwa za kweli kwani Bodi walizikana.

“Hata Polisi wameangalia hizo risiti wamethibitisha kuwa hizo risiti ni feki,” alisema.

“Nilipomuuliza Hume akasema yeye huwa anamtumia wakala wake, ikiwa pamoja na kupeleka fedha, kwa hiyo unaniambia (wakala) agent wangu amenidanganya? Mimi nikamwambia sijui maana wewe ndiyo uliyesema.”

Aliongeza kuwa, Hume alikuwa akikataa kabisa kumtambulisha kwa mawakala wake wa kibiashara wala kusema wanapatikana wapi.

Alisema Hume alikamatwa na Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na kuwekwa mahabusu kwa siku tano kisha akaachiwa.

Hume alipoulizwa na Mwananchi kwa simu alisema, “hilo suala liko Polisi, siwezi kulizungumzia.”

Mlalamikaji huyo amedai kutoa zaidi ya Dola479,500 katika nyakato tofauti, huku mbia wake Hume akidai kutoa malipo ya awali ya Dola 150,000.

Mwananchi limefanikiwa kuuona mmoja wa mikataba iliyoingiwa kati ya kampuni ya Eagle Investment and Logistics (T) Ltd na chama cha Ushirika cha Liwale ambao walikubaliana kuuziana tani 1,000 za korosho kwa msimu wa 2017/18 kwa bei ya Dola 1,320 kwa kilo, Februari 2018.

Mkataba mwingine ambao Mwananchi limeuona ni kati ya Eagle Investment and Logistics (T) Ltd iliyodaiwa kuiuzia Raj Dry Fruits Traders tani 1,000 za korosho uliosainiwa Februari 28, 2018.

Mmoja wa wanasheria wa kampuni ya FK Law Chambers iliyosimamia mchakato wa ‘ununuzi wa korosho’ na ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema upotevu huo wa fedha ulisababishwa na mteja wao kumwamini sana Hume.