Kampuni ya Mwananchi kuwalipa mshahara wa mwaka mzima wakunga wawili

Mkurugenzi Mtendaji wa MCL Francis Nanai akizungumza kwenye mkutano huo.

Muktasari:

  • Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) itatoa msaada wa kuwalipa mshahara wa mwaka mzima wakunga wawili ili kusaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Dar es Salaam. Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) itatoa msaada wa kuwalipa mshahara wa mwaka mzima wakunga wawili ili kusaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto.

MCL imeeleza hayo leo Jumamosi Mei 4 wakati shirika la Amref Health Africa lilipokutana na wakurugenzi wa kampuni mbalimbali kuangalia namna ya kusaidia kupata mishahara ya wakunga ambao limewapatia mafunzo.

Akizungumza kwenye mkutano huo,  Mkurugenzi Mtendaji wa  MCL, Francis Nanai alisema kwa kuanzia  watasaidia kuwalipa mishahara ya mwaka mzima wakunga wawili ambao kila mmoja anahitaji kiasi cha dola 2,500 za Marekani ambazo sawa na  Sh6 milioni.

Amesema kufanya hivyo siyo tu ni jambo, bali pia inasaidia kueleweka kwa kampuni na kuonyesha kwa vitendo ni namna gani inasaidia jamii.

"Idadi kubwa ya vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua kama inavyoelezwa na wataalamu hapa ni kubwa, inauma na inasikitisha, wito wangu kwa wadau wengine zikiwamo kampuni mbalimbali kuunga mkono suala la kusaidia sekta hii muhimu kwa ustawi wa kizazi kijacho," alisema Nanai.

Naye, Naibu Waziri wa Afya,  Dk Faustine Ndugulile alisema changamoto inayoikabili sekta ya afya ni rasilimali watu, ambapo kwa sasa Serikali imefikia asilimia 50 ya watumishi wote wanaohitajika.

Amesema mkakati uliopo ni kuhakikisha wanapatikana watumishi wa ziada hususan wakunga.

Amesema kwa mujibu wa takwimu zilizopo kina mama 11,000 hufariki kila mwaka kutokana na matatizo ya uzazi, ikimaanisha 30 hufariki kila siku katika vizazi hai 100,000.

"Nimefarijika kuona sekta binafsi inajitokeza kuchangia katika sekta ya afya, mchango wao utasaidia kupunguza tatizo la wakunga wanaosubiri ajira ambao wameshapewa mafunzo na Amref kama ambavyo wengine wameahidi kufanya hivyo" amesema.

 Dk Ndugulile amesema kila mkunga mmoja watakayemuajiri anakwenda kuhudumia kina mama 500 kwa mwaka na kwamba  huo ni mchango mkubwa kwenye sekta ya afya na jamii kwa ujumla.

“Kumuweka mkunga mwenye weledi kwenye kituo, zanahati au hospitali kunapunguza vifo vya watoto  vitokanavyo na uzazi kwa asilimia 43 na vya mama wanaojifungua kwa asilimia 67.”

"Mkutano huu umekuja wakati muafaka ambapo kesho nitakuwa Simiyu kwenye maadhimisho ya siku ya wakunga yanayofanyika huko kitaifa, miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa ni pamoja na kuhakikisha hakuna vifo vya mama na mtoto kwa sababu mimba siyo ugonjwa" amesema Dk Ndugulile.

Naye Mkurugenzi Mkaazi wa Amref Africa, Dk Florence Temu amesema Juni 29 mwaka huu watakuwa na matembezi ya hisani kusaidia ajira kwa wakunga waliohitimu masomo ngazi ya cheti ambao hawapo kwenye ajira rasmi.

Amesema wameshatoa mafunzo kwa wakunga 383 wa ngazi ya cheti tangu mwaka 2013, kati yao 327 wamepata vyeti na walioajiriwa ni 199, hivyo 208 hawana ajira ndiyo sababu ya kukusanya fedha hizo ili kuwawezesha kuajiriwa.

Amesema wamelenga kukusanya Sh 150 milioni ambapo katika matembezi ya hisani watanunua tiketi kwa Sh 25,000.

Kwa upande wake, mkurugenzi mkazi wa Trade Mark Afrika Mashariki, John Ulanga amesema hilo ni tatizo kubwa hivyo wanaziomba taasisi, kampuni binafsi kushirikiana na Amref inayoshirikiana na wizara ya afya kutatua changamoto hiyo.

"Kwa leo tu zaidi ya Sh 50 milioni zimeahidiwa, hivyo kwa kuanzia ni hatua nzuri," amesema Ulanga.