Kamwelwe azitafutia tenda ya kusafirisha samaki ndege za ATCL

Muktasari:

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe leo Jumanne amefanya ziara katika viwanda vya uzalishaji mabondo na kuchakata minofu ya samaki jijini Mwanza.


Mwanza. Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe ameanza kutafuta fursa za ndege za Serikali ambazo zimekodishwa kwa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kwa kufanya ziara katika viwanda vya uzalishaji mabondo na kuchakata minofu ya samaki jijini Mwanza.

Akizungumza baada ya kufika ofisi za kanda rasilimali za uvuvi jijini hapa leo Jumanne Januari 15, 2019, Waziri Kamwelwe amesema lengo la ziara yake ya siku moja ni kuangalia mzigo unaozalishwa na viwanda hivyo ili kuandaa mazingira mazuri kwa ajili ya kusafirisha bidhaa hizo nje ya nchi kupitia usafiri wa anga kwa kutumia shirika la ndege la ATCL.

"Juzi tarehe 12 Waziri Luhaga Mpina (mifugo na uvuvi) alinipigia simu akanieleza kwamba kuna mzigo mkubwa wa minofu na mabondo, hivyo nimekuja kujionea viwanda vilivyopo na uwezo wake wa kuzalisha mzigo,” amesema.

Waziri huyo amesema pia atatamani kuangalia na machinjio ya mbuzi kuona kiwango kinachozalishwa.

Amesema kila baada ya siku saba huwa anatembelea Bandari ya Dar es Salaam ambapo hushushwa makontena 7,000 kutoka nje ya nchi lakini hurudi yakiwa matupu bila mzigo hivyo wanataka kuondoa hali hiyo.

"Baada ya ziara yangu Mwanza nitaenda Kanda ya Mbeya kuangalia uzalishaji wa mbogamboga kisha nitaenda kanda za Arusha na Kilimanjaro kuangalia mashamba ya maua,” amesema.

Naye ofisa mfawidhi rasimali za uvuvi Ziwa Victoria, Didas Mtambalike amesema wameandaa viwanda tisa vinavyozalisha minofu na mabondo atakavyotembelea.