Kapteni wa Zimamoto, wenzake kizimbani kwa kuvua samaki eneo la hifadhi

Monday February 11 2019

By Pamela Chilongola, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Kapteni wa Zimamoto, Selemani Ally na wenzake watatu wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka mawili likiwamo la kuvua samaki kwenye eneo la hifadhi ya bahari Bougoyo.

Washtakiwa wengine ni Hifadhi Khamisi, Said Imani na Mohamed Njugu.

Mwendesha mashitaka, Groria Mwenda, akisoma hati mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustino Rwezile leo Jumatatu Februari 11, 2019 amedai katika shtaka la kwanza washtakiwa kwa pamoja kati ya Julai 11, 2018 maeneo ya hifadhi ya bahari Bougoyo jijini Dar es Salaam walikutwa wakimiliki vifaa vya uvuvi huku wakijua ni kosa la kisheria.

Katika shtaka la pili washtakiwa kwa pamoja Julai 11, 2018 katika maeneo ya hifadhi ya bahari Bougoyo jijini Dar es Salaam walikutwa wakivua samaki huku wakijua kufanya hivyo ni kosa la kisheria.

Mwenda alidai kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na aliiomba mahakama ipange tarehe nyingine ya kutajwa.

Baada ya kusomewa washtakiwa kwa pamoja walikana mashtaka yote yanayowakabili.

Hakimu Rwezile alisema dhamana ipo wazi kwa washitakiwa ingawa wanatakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye barua zinazotoka taasisi zinazotambulika watakaosaini bondi ya Sh5 milioni kila mmoja.

Mshtakiwa wa kwanza Ally alishindwa kutimiza masharti ya dhamana amerudishwa rumande wakati wenzake watatu wametimiza masharti na wapo nje kwa dhamana.

Rwezile ameahirisha shauri hilo hadi Machi 6, 2019 kesi hiyo itakapotajwa tena.

Advertisement