Kapuya: Sijafanya kosa kuoa binti

Muktasari:

Mapema wiki  hii picha na video za harusi ya mwanasiasa huyo mkongwe zilizua gumzo mitandaoni kutokana na tofauti yao ya umri

 


Dar es Salaam. Aliyekuwa mbunge Urambo Magharibi (CCM), Profesa Juma Kapuya amesema hajavunja sheria wala kukiuka taratibu zozote kumuoa mwanamke aliyemzidi umri.

Mapema wiki  hii picha na video za harusi ya mwanasiasa huyo mkongwe zilizua gumzo mitandaoni kutokana na tofauti yao ya umri.

Akizungumza leo Alhamisi Februari 21, 2019 Kapuya mwenye umri wa miaka 73 amesema anashangaa ndoa yake na Mwajuma Mwiniko anayedaiwa kuwa na miaka 25,  kuzua gumzo wakati hajavunja sheria au kukiuka taratibu zozote za nchi.

“Kwani wanataka nioe mwanamke mwenye umri sawa na bibi yangu,” amehoji.

Kapuya amesema umri hauhusiani na mapenzi, hivyo watu wakubali matokeo kwani hajamtorosha shule mwanamke huyo, wala hajavunja sheria, mila, desturi au misingi  ya dini.

“Nimevunja sheria, nimekiuka maadili, nimemuachisha shule  Hapana,” amesema  Kapuya ambaye pia amewahi kumiliki bendi maarufu ya muziki wa dansi ya Akudo.

Waziri huyo wa zamani wa Elimu amesema Mwajuma ni mkewe wa pili na kubainisha kuwa hataongeza mwingine.

“Siwezi tena kuoa mwanamke mwingine kwani mke huyu ni somo tosha, sababu mke wangu wa kwanza anaishi Dar es Salaam na nampenda sana. Hapa subirini tu mtoto kutoka kwa huyu mwanamke mnayesema ana umri mdogo," amesema Kapuya.

Akizungumzia alivyokutana na mkewe, Kapuya amesema alimfahamu alipokuwa anakwenda kufanya vikao akitokea Urambo.

Amsifu anajua kupika

Profesa Kapuya amesema akifika Dar es Salaam  atamkaribisha chakula kilichopikwa na mkewe akimsifu kuwa mtaalamu wa katika masuala hayo.

“Nikifika Dar nitakualika, anajua kupika balaa. Utafurahia,” amesisitiza.