VIDEO: Kapuya awatwanga maswali manne wanaohoji ndoa yake

Dar es Salaam. Mapema wiki hii, picha na video za harusi za mwanasiasa mkongwe aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Urambo Magharibi, Profesa Juma Kapuya zilizua gumzo mitandaoni kutokana na tofauti yao ya umri.

Mwananchi jana lilimtafuta Profesa Kapuya ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 73 na kuzungumza naye kuhusu ndoa yake kwa Mwajuma Mwiniko anayedaiwa kuwa na miaka 25.

“Nimevunja sheria, nimekiuka maadili, nimemuachisha shule? jibu ni hapana, sasa wanataka kunituhumu kwa kipi,” alihoji Kapuya ambaye pia aliwahi kuwa waziri katika wizara kadhaa nchini.

Mbali ya maswali hayo, profesa huyo pia aliwauliza wanaomshangaa kuoa mwanamke aliyemzidi umri akisema, walitaka aoe mwanamke mwenye umri sawa na bibi yake?

Alisema umri hauhusiani na mapenzi, hivyo watu wakubali matokeo kwa sababu hajamtorosha shuleni binti huyo wala hajavunja sheria, mila, desturi au misingi ya dini yake.

Kapuya ambaye pia katika miaka ya 1990 alikuwa mmiliki wa bendi maarufu ya muziki wa dansi ya Akudo Impact alisema siyo sahihi kwa watu kuzungumzia mambo ambayo hawayafahamu hasa yanayohusu faragha za wengine.

Alisema Mwajuma anakuwa mke wake wa pili na kwamba hataongeza mwingine. “Siwezi tena kuoa mwanamke mwingine kwa sababu mke huyu ni somo tosha, mke wangu wa kwanza anaishi Dar es Salaam naye nampenda sana. Hapa subirini tu mtoto kutoka kwa huyu mwanamke mnayesema ana umri mdogo,” alisema Kapuya.

Akizungumzia alivyokutana na mke wake huyo mpya, Profesa Kapuya alisema alimfahamu binti huyo ambaye ni mwenyeji wa Kaliua, mkoani Tabora alipokuwa anaenda kufanya vikao ambavyo hata hivyo, hakuvitaja ni vya nini akitokea Urambo.

Mwajuma anajua kupika

Profesa Kapuya ambaye pia aliwahi kuwa waziri wa elimu, waziri wa kazi na waziri wa ulinzi alimuahidi mwandishi wetu, “nikifika Dar es Salaam, nitakukaribisha chakula kilichopikwa na mke wangu Mwajuma ni mtaalamu katika mapishi.

“Anajua kupika balaa. Yaani anapika huyo si mchezo, utafurahi mwenyewe.”

Kuhusu siasa

Akizungumzia siasa, Profesa Kapuya alisema tangu aliposhindwa katika Uchaguzi Mkuu uliopita mwaka 2015 aliamua kujiweka kando.

Katika uchaguzi huo, Profesa Kapuya alipitishwa na Chama cha Mapinduzi kugombea Jimbo la Urambo Magharibi lakini alipigwa mwereka na Magdalena Sakaya aliyesimama kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF).

Alisema baada ya kushindwa katika uchaguzi huo, aliamua kufanya shughuli zake nyingine na hadi sasa hajawahi kujihusisha tena na masuala ya siasa.

“Mwaka 2015 niliposhindwa kupata ubunge, niliridhika nikaamua kupumzika na kwa sasa muda mwingi nakuwa niko Dar es Salaam. Sikutaka kulalamika au kwenda mahakamani ila mpaka sasa sijaamua kama nirudi kwenye siasa ama la,” alisema Kapuya.