Katibu wa Nyerere afariki

Aliyewahi kuwa Katibu wa Baba wa Taifa, mwalimu Julius Nyerere, mzee Laurent Batao (83) amefariki dunia kijijini kwake Bugombe kata ya Kanyigo Wilaya ya Missenyi, mkoani Kagera.

Muktasari:

  • Laurent Batao, aliyekuwa miongoni mwa makatibu wa Baba wa Taifa, mwalimu Julius Nyerere, amefariki dunia akitibiwa Hospitali Teule ya Mugana wilayani Missenyi na mazishi yanatarajiwa kufanyika Jumamosi kijijini kwake Bugombe

Bukoba. Aliyewahi kuwa Katibu wa Baba wa Taifa, mwalimu Julius Nyerere, mzee Laurent Batao (83) amefariki dunia kijijini kwake Bugombe kata ya Kanyigo Wilaya ya Missenyi, mkoani Kagera.

Mtoto wa marehemu, Mugisha Batao amesema leo Alhamisi Aprili 25, 2019 kuwa baba yake amefariki jana akipatiwa matibabu katika Hospitali Teule ya Mugana na mazishi yanatarajiwa kufanyika Jumamosi hii.

Kwa mujibu wa mtoto wake, baada ya mwalimu Nyerere kung'atuka madarakani baba yake aliendelea kuishi Butiama mkoani Mara kwa miaka kadhaa baadaye alirejea kijijini kwao Bugombe wilayani Missenyi.

Mugisha amesema miongoni mwa waliojulishwa kuhusu kifo hicho ni mjane wa mwalimu Nyerere, mama Maria.

Pia, amesema Batao ameacha watoto 12 na alifanya kazi na mwalimu Nyerere takriban kwa miaka 20.

Akizungumzia kifo hicho, mkazi wa kijiji cha Bugombe, Dasianus Karaba ambaye alikuwa mfanyakazi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, amesema alimfahamu wakati wa ziara za mwalimu Nyerere jijini Nairobi nchini Kenya.

Pia, amesema Batao alikuwa na maktaba nyumbani kwake na mara kadhaa alikwenda kuazima vitabu.