Katibu wakuu watia timu mgodi wa Acacia, kutoka na maagizo

Wednesday January 9 2019

By Beldina Nyakeke, Mwananchi [email protected]

Tarime. Timu ya Makatibu wakuu watano kutoka katika wizara tano ikiwemo wizara ya madini pamoja na mazingira wanafanya ziara katika mgodi wa dhahabu wa Acacia North Mara wilayani Tarime.

Pamoja na mambo mengine timu hiyo inatarajiwa kutoa tamko juu ya tuhuma za utiririshaji wa maji ya sumu zinazoukabili mgodi huo.

Timu hiyo ikiongozana na katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Carolina Mthapula na baadhi ya maofisa kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa Mara imewasili leo Jumatano Januari 9, 2019 mgodini hapo na kufanya ukaguzi wa sehemu mbalimbali ikiwemo bwawa la maji machafu (TFS) na miundombinu yake namna inavyofanya kazi.

Baada ya ukaguzi huo timu hiyo imejifungia ndani kwa zaidi ya saa mbili na uongozi wa mgodi huo kwaajili ya majadiliano kabla ya kutoa taarifa kwa vyombo vya habari juu ya madhumuni ya ziara hiyo ya siku moja.

Hata hivyo, habari ambazo hazijathibitishwa zinadai pamoja na mambo mengine timu hiyo imefika mgodini hapo kwaajili ya kufuatilia utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli juu ya ulipwaji wa fidia kwa wakazi wa vijiji vinavyozunguka mgodi huo ambao maeneo yao yamechukuliwa na mgodi ili kupisha shughuli za uchimbaji.

Septemba mwaka jana akiwa mkoani Mara, Rais Magufuli aliziagiza mamlaka zinazohusika kuhakikisha wananchi wanaodai fidia mgodini hapo waweze kulipwa na kupisha kwa maelezo kuwa tathmini ilikwisha fanyika lakini utekelezaji ulishindikana bila sababu za msingi.

Advertisement