Katumbi Bilionea aliyemnyima usingizi Kabila, atikisa DRC

Muktasari:

Utawala wa Rais mstaafu wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Joseph Kabila ulishuhudia wapinzani wake wengi wakifunguliwa mashitaka na kufungwa huku wengine wakikimbilia uhamishoni.

Utawala wa Rais mstaafu wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Joseph Kabila ulishuhudia wapinzani wake wengi wakifunguliwa mashitaka na kufungwa huku wengine wakikimbilia uhamishoni.

Wachambuzi waliitafsiri hatua hiyo kama janja ya kiongozi huyo kuendelea kubaki madarakani, hivyo mbinu ya kuwanyamazisha watu aliowaona ni tishio kwa utawala wake ingweza kumfaa. Hata hivyo, nguvu ya umma na shinikizo la jumuiya ya kimataifa lilimfanya aondoke miaka miwili baada ya kumaliza muda wake wa kikatiba.

Miongoni mwa watu walioguswa na mkono wa Kabila, ni mwanasiasa na mfanyabiashara maarufu nchini humo, Moise Katumbi (54). Tangu bilionea huyo alipotangaza kuwania urais mwaka 2015, alianza kuandamwa.

Mwishowe Katumbi akaondoka nchini humo na kwenda kuishi uhamishoni Afrika Kusini na Ubelgiji kwa takribani miaka mitatu iliyopita baada ya kushtakiwa na Serikali ya Rais Kabila kwa makosa kadhaa ya uhalifu ikiwamo udanganyifu, kuajiri raia wa kigeni na kujipatia uraia wa pili kinyume cha sheria.

Mwaka 2016, Katumbi alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela kwa kununua nyumba kinyume cha sheria huko Lubumbashi, pia kuwaajiri raia wa kigeni ili kupanga njama dhidi ya Serikali.

Baada ya hukumu hiyo, Katumbi alikimbilia Afrika Kusini ambako aliishi kabla ya kwenda Ubelgiji. Mwaka 2018, alijaribu kurejea DRC kupitia Zambia ili kwenda kujiandikisha kama mgombea wa urais, hata hivyo, alizuiliwa kuingia nchini humo.

Tshisekedi atoa msamaha

Baada ya uchaguzi wa Desemba 30, 2018 na Felix Tshisekedi kuibuka mshindi baadae kuapishwa kuiongoza nchi hiyo, kiongozi huyo mpya alitangaza kuwaachia huru wafungwa wote wa kisiasa na kuwaita nyumbani wanasiasa wanaoishi uhamishoni.

Rais Tshisekedi alianza kutekeleza ahadi mbalimbali alizoziahidi ndani ya siku 100. Kati ya hizo ni kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa ambao wengi wao walifungwa wakati wa utawala wa miaka 18 ya Kabila.

Rais huyo amewaachia huru mamia ya wafungwa hao ambapo kati yao wamo wanasiasa maarufu nchini humo kama vile Frank Diongo, Diomi Ndongala na Firmin Yangambi ambao walishitakiwa kwa makosa ya kutishia usalama wa Taifa.

Ahadi nyingine ya Tshisekedi ni kufungua uwanja wa demokrasia kwa vyama vya upinzani ambavyo kwa muda mrefu vililalamia kukandamizwa na Serikali ya Kabila.

“Nitafanya kazi kwa bidii kuhakikisha tunatengeneza mazingira ambayo yatawawezesha Wacongo wote wanaoishi nje ya nchi kwa sababu za kisiasa kurejea nyumbani haraka na kuendelea na shughuli zao kwa mujibu wa sheria,” aliahidi Tshisekedi Machi mwaka huu.

Kauli hiyo ya Tshisekedi imemvuta Katumbi kurejea nyumbani ambako amejenga ngome ya kibiashara na kisiasa. Hakujiuliza mara mbili kuhusu kurejea nyumbani, mara moja akachukua hatua na kurudi DRC.

Arejea kwa kishindo

Taarifa za kurejea DRC zilitangazwa Mei 6, mwaka huu na kituo cha televisheni cha France24 cha Ufaransa. Katumbi alinukuliwa na kituo hicho akisema “ni hakika kwamba Mei 20, nitakuwa Lubumbashi.”

Mei 20, Katumbi alilakiwa uwanja wa ndege wa Luano mjini Lubumbashi na maelfu ya wafuasi wake ambao walijawa na furaha kumuona tena baada ya miaka mitatu ya kuwa uhamishoni.

Katumbi aliwasili Lubumbashi kwa ndege yake binafsi akiwa amevalia mavazi meupe. Akiwa ubelgiji, alinukuliwa na Shirika la Habari la AFP akisema kwamba aliiandikia mamlaka ya usafiri wa anga ya DRC akiomba kibali cha kutua Lubumbashi kwa ndege binafsi.

Ujio wake ulipokelewa kwa shangwe ambapo umati wa watu ulimsindikiza Katumbi kuelekea katika uwanja wa michezo wa klabu ya TP Mazembe ambayo anaimiliki. Wakati akielekea uwanjani, alipanda gari la wazi na kupunga mkono kwa maelfu ya wananchi walioandamana naye na kuamsha shangwe.

“Maelfu wamejitokeza uwanja wa ndege kumpokea Katumbi. Ameamsha ari ya kisiasa. Amesema atasajili chama chake cha siasa na kuzunguka nchi nzima kunadi sera zake,” anasema mwandishi wa habari wa Al-Jazeera, Catherine Wambua-Soi.

Mmoja wa wananchi waliojitokeza kumpokea Katumbi, Solange Milongo alinukuliwa na Shirika la Habari la BBC akisema Katumbi ni mtoto wa Lubumbashi, hivyo wanampa heshima zote kama kiongozi wao ambaye wamemkosa kwa miaka miatatu. Uwepo wake ni muhimu kwa uchumi na ajira kwa Wacongomani “Ujio wake leo unatikisa DRC yote, kila mmoja anafahamu na kufurahi”.