Kauli ya Nape kuhusu Bunge Live kupigwa kufuli yaibua mjadala

mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye 

Muktasari:

Nape alipokuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo aliweka msimamo wa Serikali kuhusu kutorushwa moja kwa moja kwa matangazo hayo ya Bunge, lakini jana wakati akihojiwa katika kipindi cha 360 kinachorushwa na Televisheni ya Clouds, alionekana kupingana na uamuzi huo.

 


Dar es Salaam. Wasomi wamesema mawaziri wengi waliopo madarakani hujikuta wanatoa matamko au kauli zilizo kinyume na matakwa yao kwa lengo la kulinda maslahi binafsi, ya Serikali na chama.

Wametoa kauli hiyo leo Jumanne Februari 19, 2019 walipoulizwa kuhusu kauli ya mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye kuhusu kusitishwa kwa matangazo ya moja kwa moja ya Bunge.

Nape alipokuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo aliweka msimamo wa Serikali kuhusu kutorushwa moja kwa moja kwa matangazo hayo ya Bunge, lakini jana wakati akihojiwa katika kipindi cha 360 kinachorushwa na Televisheni ya Clouds, alionekana kupingana na uamuzi huo.

Aprili 25, 2016 jijini Dodoma, akiwa Waziri mwenye dhamana ya habari Nape alijikuka katika wakati mgumu baada ya kuzomewa na wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wakati akitetea hoja ya Serikali ya kutokurusha matangazo hayo moja kwa moja.

Katika kipindi hicho cha jana Nape amesema si yeye aliyeanzisha ajenda ya kuua matangazo hayo bali ilikuwapo tangu Bunge la 10.

Wakizungumzia kauli hiyo ya Nape, Richard Mbunda wa Idara ya  Sayansi ya Siasa na Utawala Bora  katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) amesema kwa wakati huo Nape alikuwa akitekeleza maagizo ya Serikali.

“Inawezekana alitekeleza bila hata yeye kupenda, sasa ukiona anatoka nje(ya uwaziri) anaongea kinyume na alichokitekeleza basi inatoa ushahidi kwamba alitekeleza kitu ambacho yeye mwenye alikuwa hakiamini,” amesema Dk Mbunda.

Amesema haitakuwa sahihi kumtupia lawama Nape licha ya kutekeleza uamuzi ulioonekana kuwa na udhaifu.

“Haitakuwa sawa tukisema libakie tatizo kwake moja kwa moja, hata yeye ni binadamu, pengine alikuwa na maoni binafsi lakini halikukubalika,” alisema.

Mwanaharakati wa haki za Kiraia na Haki za Binadamu, Gemma Akilimali amesema changamoto aliyokutana nayo Nape iwe fundisho kwa mawaziri wengine wanaofanya kazi na Serikali kuhakikisha wanaishi na kusimamia wanachokiamini katika nafasi zao hata baada ya kuondoka madarakani.

“Tatizo wanashindwa kuwa wazi(mawaziri) kabla ya kuteuliwa kwao, lazima waangalie kama majukumu wanayopewa yanaweza kuathiri misimamo yao ya kiuongozi, Nape alikubali kutekeleza uamuzi ambao hakukubaliana nao, “amesema Gemma.