Kauli ya polisi Kigoma kuhusu wabakaji wa ‘teleza’

Martin Ottieno

Muktasari:

Wakati habari za wanaume wanaojipaka oil chafu maarufu ‘wanaume teleza’ kisha kuwabaka wanawake mkoani Kigoma zikitikisa nchini Tanzania, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Martin Ottieno amesema watu hao ni wahalifu.

Kigoma. Wakati habari za wanaume wanaojipaka oil chafu maarufu ‘wanaume teleza’ kisha kuwabaka wanawake mkoani Kigoma zikitikisa nchini Tanzania, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Martin Ottieno amesema watu hao ni wahalifu.

Vitendo mbalimbali vinavyofanywa na ‘wanaume teleza’ mkoani humo vimezungumzwa mara kadhaa na Mei 20, 2019 bungeni jijini Dodoma mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo),  Zitto Kabwe alitoa maelezo kuhusu vitendo vinavyofanywa na kundi hilo ikiwa ni pamoja na kubaka, kujeruhi na kuiba.

Zitto alisema shirika lisilo la kiserikali la Tamasha, wamekusanya matukio ya wanaume teleza na kubaini matukio kama 43.

Katika maelezo yake kwa Mwananchi jana Mei 22, 2019 Kamanda Ottieno amekiri kuwepo vitendo vya baadhi ya vijana kuvunja nyumba za watu na kujeruhi.

Amesema mwaka  2019 yameripotiwa matukio manne yanayohusisha vijana kuvunja, kujeruhi na kuiba na kwamba watu watatu wanashikiliwa na polisi kwa mahojiano.

"Jamii itambue watu wanaojiita teleza ni wahalifu sugu wanaovunja na kuiba. Jamii lazima ishirikiane na vyombo vya dola kutokomeza vitendo vya uhalifu," amesema Ottieno.

Ametoa mwito kwa taasisi na watu wengine kufika Polisi kwa ajili ya kupata ufafanuzi wa mambo yanayohusiana na vitendo vya uhalifu badala ya kuandika taarifa za upande mmoja kwa vile sheria ya takwimu inakataza kutoa taarifa bila uthibitisho wa mamlaka husika.

Wakati Kamanda Ottieno akieleza hayo Mwananchi limezungumza na baadhi ya wakazi wa mkoani Kigoma kuhusu matukio hayo.

Mkazi wa Katubuka, Lucy Daudi amesema mwaka 2017 akiwa amelala nyumbani kwake alishtuka na kukuta mtu akimpapasa mwilini na alipopiga kelele kuomba msaada mtu huyo alimjeruhi kichwani na kitu chenye ncha kali.

Amesema mtu huyo alikimbia na kwamba tukio hilo hakuripoti sehemu yoyote.

Mkazi wa Mwanga mkoani humo,  Hussein Rajabu amedai  baadhi ya vijana wanaofanya uhalifu pia hutumia nafasi hiyo kuwabaka wanawake kwa kuamini wakifanya hivyo hawawezi kukamatwa maana wanawake hawawezi kupiga kelele kuomba msaada kwa majirani.

Naye Fausta Stefano amesema kwa sasa wanawake kuvamiwa nyumbani na kubakwa na watu wanaojiita teleza vimepungua si kama miaka ya nyuma.

Alichokisema Lugola kuhusu teleza

Akijibu hoja ya Zitto bungeni, Waziri wa Mambo ya Ndani Kangi Lugola alisema ubakaji ni kosa la jinai na linaadhibiwa kisheria na kwamba vitendo hivi vya makosa ya aina hii vimekuwa vikitokea si Kigoma tu hata maeneo mengine na vimekuwa vikidhibitiwa.

“Kwa mkoa wa Kigoma, matukio aliyosema Zitto ni kweli vinadhalilisha na walikuwa wanajikuta mtu ambaye haonekani kwa macho na mwanamama anajikuta sehemu zake za siri amelowa,” amesema Lugola na kuongeza kuwa mwanamke akitaka kumshika mtu huyo analeteza.

“Vitendo hivi vimeendelea kudhibitiwa na nilipopata taarifa kutoka kwa Zitto na mkurugenzi wa Twaweza, Aidan Eyakuze. Lakini jambo hilo si kubwa kwa kiasi hicho, kama anavyosema Zitto, tukiangalia taarifa katika vitabu vyetu pale Kigoma, hakuna taarifa zilizoripotiwa mpaka leo,” amesema waziri huyo ambaye pia ni mbunge wa Mwibara (CCM).

Amesema katika kipindi cha mwaka mmoja, hakuna tukio lolote lililohusisha mwanamke kubakwa isipokuwa yapo matukio matatu ya kubakwa yanayohusisha wanawake kujeruhiwa katika nyumba zao.

Waziri Lugola amesema yawezekana katika kujeruhiwa hawakufikia kiwango cha kutenda kosa.

“Kwenye maeneo mbalimbali katika nchi yetu, kuna baadhi ya taasisi au mtu mmoja mmoja, wanakuza mambo na kujenga hofu, niseme bayana, taasisi ambazo zinakwenda kufanya tafiti na kukuza mambo, tumeanza kuziorodhesha na hatua zitaanza kuchukuliwa,” amesema Lugola.

Wakati wote huo, Zitto alikuwa akisimama mara kwa mara kutaka kuzungumza lakini Mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga alimzuia akimtaka kusubiri waziri amalize kisha atampa nafasi ya kuzungumza.

“Kama Zitto una taarifa hizo, niko tayari kwenda Kigoma na nitachukua hatua,” amesema Waziri Lugola.