Kenya, Somalia katika mzozo mkali

Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta (kushoto) akipeana mkono na Balozi wa Somalia nchini humo, Mahmoud Ahmed Nur katika hafla ya kupokea hati ya utambulisho wake nchini humo, Desemba 5, 2018.

Muktasari:

Mgogoro huo umekuja baada ya madai kwamba Somalia imepiga mnada vitalu vya mafuta vilivyopo katika eneo la Bahari ya Hindi ambalo Kenya inadai ni sehemu yake huku Kenya ikidaiwa kumfukuza balozi wa Somalia na kumtaka balozi wake nchini Somalia arudi nyumbani.

Dar es Salaam. Kenya na Somalia zimeingia kwenye mgogoro wa kidiplomasia.

Mgogoro huo umeibuka baada ya Somalia kudaiwa kupiga mnada vitalu vya mafuta vilivyopo katika eneo la Bahari ya Hindi ambalo Kenya inadai ni sehemu yake.

Juzi, Kenya ilimfukuza Balozi wa Somalia nchini humo, Mahmoud Ahmed Nur kutokana na sababu hiyo. Somalia inadaiwa kupiga mnada vitalu hivyo Februari 7 huko Uingereza jambo ambalo Kenya imeliita kuwa ni kuingilia mambo yake ya ndani.

Mbali na kumfukuza balozi huyo, Kenya imemwita nyumbani balozi wake aliyepo Somalia, Lucas Tumbo kwa mashauriano zaidi kuhusu suala hilo huku ikisema imejiandaa kulinda mipaka yake kwa gharama yoyote.

Taarifa iliyotolewa na Serikali ya Kenya juzi imeeleza kwamba eneo hilo ni la kwake na kwamba imepita njia mbalimbali za usuluhishi kati yake na Somalia ikiwamo Mahakama ya Kimataifa (ICJ).

Serikali ya Kenya imeeleza kwamba kwa zaidi ya miaka 30 imekuwa ikihifadhi maelfu ya wakimbizi kutoka Somalia na mpaka sasa inahifadhi Wasomali wengi licha ya kukabiliwa na wizi na matukio ya kigaidi na kusisitiza kwamba haitaruhusu hali hiyo kuendelea na kwamba uvumilivu wa watu wa Kenya umekwisha.

Hata hivyo, taarifa hiyo haijafafanua hatua ambazo nchi hiyo itachukua kukabiliana na suala hilo.

Kenya imekuwa ikikabiliwa na mashambulizi ya kigaidi ambayo yanadaiwa kufanywa na kikundi cha Al Shaabab ambacho kina maskani yake Somalia. Pia, Kenya ina hifadhi wakimbizi takriban 400,000 katika kambi yake ya Dadaab, wengi wao wakiwa ni Wasomali.

Mwanasia mkongwe wa Kenya, Musalia Mudavadi ameitaka jumuiya ya kimataifa kuingilia kati suala hilo akisema linaweza kusababisha matatizo makubwa baina ya mataifa hayo mawili ikiwamo uvunjifu wa amani.

“Hatutaki kuukuza mgogoro huu. Sisi kama Wakenya tunapata shida kutokana na madhara kutoka kwa hawa majirani zetu. Tumeshuhudia ndugu zetu wakipoteza maisha kwenye mashambulizi ya kigaidi,” alisema Mudavadi ambaye aliwahi kuwa Makamu wa Rais wa Kenya mwaka 2002 na Naibu Waziri Mkuu kuanzia mwaka 2008 mpaka 2012.