Kesi mauaji Scolastica kusikilizwa mfululizo

Edward Shayo ambaye ni mshtakiwa namba mbili katika kesi ya mauaji ya mwanafunzi wa Sekondari ya Scolastica, Humphrey Makundi akishuka kwenye gari la polisi baada ya kufikishwa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Muktasari:

Yapangiwa Jaji Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi,

mashahidi 34 kutoa ushahidi

Moshi. Kesi ya mauaji ya mwanafunzi wa kidato cha pili wa Sekondari ya Scolastica, Humphrey Makundi, imepangwa kusikilizwa mfululizo kuanzia Aprili 2 na jaji kutoka nje ya mkoa wa Kilimanjaro.

Kesi hiyo inayovuta hisia za wakazi wengi wa ndani na nje ya mkoa wa Kilimanjaro, inamkabili mmiliki wa shule hiyo, Edward Shayo, mwalimu wa nidhamu Labani Nabiswa na mlinzi wa shule, Hamis Chacha.

Taarifa ya Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi Frank Mahimbali, ilieleza kesi hiyo itasikilizwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi Dar es Salaam, Firmin Matogolo.

Naibu msajili huyo aliwatumia taarifa ya maandishi mawakili wa Divisheni ya Taifa ya Mashtaka (NPS) na wale wa jopo la utetezi, Elikunda Kipoko, David Shillatu na Patrick Paul, kuwataka wafanye maandalizi.

“Kesi tajwa (CC 48/2018) imepangwa kuanza kusikilizwa mfululizo kuanzia Aprili 2 (2019) mbele ya mheshimiwa Jaji Matogolo. Kwa barua hii mnatakiwa kufanya maandalizi ya kuanza kwa kesi hii,” alieleza.

Wakati wa usikilizwaji wa awali Agosti 27, 2018 mbele ya Jaji Haruna Songoro, upande wa mashtaka ukiongozwa na wakili wa Serikali mkuu Joseph Pande, ulieleza utaita mashahidi 34 katika kesi hiyo.

Pia, Pande aliijulisha Mahakama kuwa wanatarajia kuwasilisha vielelezo vya nyaraka 15 yakiwamo maelezo ya kukiri kosa ya mshtakiwa Chacha akiwa polisi na kwa mlinzi wa amani.

Mbali na nyaraka hizo, watawasilisha taarifa ya mawasiliano ya simu kutoka kampuni ya Vodacom inayodaiwa kuonyesha washtakiwa waliwasiliana muda na siku ya mauaji.

Mbali na vielelezo hivyo, upande huo wa mashtaka ulieleza Mahakama kuwa utawasilisha vielelezo halisi (physical or real) ambavyo ni simu saba, panga moja na nguo za marehemu.

Kwa upande wa mawakili wa utetezi, wao waliiambia Mahakama kuwa orodha ya mashahidi wao pamoja na vielelezo watakavyovitumia, wataviwasilisha kabla ya washtakiwa kuanza kujitetea.

Mwanafunzi huyo alitoweka shuleni Novemba 6, 2017 na baadaye kubainika ameuawa na watu wasiojulikana baada ya maiti ya mtu aliyedaiwa ni mtu mzima mwenye ndevu, kufukuliwa kwa amri ya Mahakama.

Mwili wa mtoto huyo uliokotwa Novemba 10, 2017 katika Mto Ghona mita zipatazo 300 kutoka shuleni hapo, polisi waliouchukua waliupeleka Hospitali ya Mawenzi na kuzikwa kwa madai haukutambuliwa. Kwa kuwa mwili huo ulishaanza kuoza na ulikuwa haujatambuliwa, ulizikwa siku iliyofuata ya Novemba 11 na Manispaa ya Moshi katika makaburi ya Karanga yaliyopo mjini hapa.

Polisi waliendelea na uchunguzi na Novemba 17, 2017 Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), iliwasilisha ombi mahakamani la kufukuliwa kwa mwili huo ili uweze kufanyiwa uchunguzi.

Mahakama ilitoa kibali cha kufukuliwa kwa mwili huo na ulipofukuliwa baba mzazi, Jackson Makundi aliweza kuutambua kuwa ni wa mwanaye na Novemba 19, 2017 ukafanyiwa uchunguzi na madaktari.

Pande alieleza Mahakama kuwa katika uchunguzi wa madaktari katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, waligundua kuwa kifo cha mwanafunzi huyo kilitokana na majeraha aliyoyapata kichwani.