Kesi ofisa wa Takukuru yapigwa kalenda tena

Muktasari:

Upande wa mashtaka katika kesi aliyekuwa Mkurugenzi wa Mipango na Ufuatiliaji na Tathmini wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Kulthum Mansoor, umedai kuwa upelelezi haujakamilika.

Dar   es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Mipango na Ufuatiliaji na Tathmini wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Kulthum Mansoo, umedai upelelelezi haujakamilika.

Kulthum anakabiliwa na makosa manane likiwamo la utakatishaji wa Sh1.47 bilioni.

Wakili wa Takukuru, Ester Martine, amedai leo Alhamisi Aprili 25, 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu, Kelvin Mhina, kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutajwa.

Martine amedai upelelezi haujakamilika na kuomba mahakama hiyo ipange tarehe nyingine.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Mhina aliahirisha kesi  hadi Mei 9, 2019 itakapotajwa.

Mshtakiwa anakabiliwa na kosa la kughushi analodaiwa kutenda tarehe tofauti Januari 2013 na Mei 2018 akiwa Makao Makuu ya Takukuru jijini Dar es Salaam, alitoa barua ya ofa ikionyesha imetoka katika halmashauri ya Bagamoyo mkoani Pwani huku akifahamu kufanya hivyo ni kosa la kisheria.

Kosa la pili, tarehe tofauti kati ya Januari 2012 na Mei 2017 akiwa eneo la Upanga, mshtakiwa anadaiwa kujipatia Sh5.2 milioni kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa mtumishi wa Takukuru, Alex Mavika, kama malipo ya kiwanja kilichopo kijiji cha Ukuni wilayani Bagamoyo huku akionyesha yeye ni mmiliki akijua ni uongo.

Kosa la tatu, tarehe tofauti kama hiyo akiwa eneo la Upanga mshtakiwa alijipatia Sh3 milioni kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa mtumishi wa Takukuru, kama malipo ya kiwanja kilichopo kijiji cha Ukuni wilayani Bagamoyo huku akionyesha yeye ni mmiliki, akijua ni uongo.

Katika kosa la nne, tarehe tofauti kama hiyo akiwa eneo la Upanga jijini Dar es Salaam mshtakiwa alijipatia Sh5 milioni kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa mtumishi wa Takukuru, Gogo Migutah kama malipo ya kiwanja kilichopo kijiji cha Ukuni wilayani Bagamoyo, huku akionyesha yeye ni mmiliki akijua ni uongo.

Kosa la tano, tarehe tofauti kama hiyo akiwa eneo la Upanga jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alijipatia Sh7 milioni kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa mtumishi wa Takukuru, Ekwabi Majungu, kama malipo ya kiwanja kilichopo kijiji cha Ukuni wilayani Bagamoyo, huku akionyesha yeye ni mmiliki akijua ni uongo.

Katika kosa la sita, tarehe tofauti kama hiyo akiwa eneo la Upanga jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alijipatia Sh7 milioni kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa mtumishi wa Takukuru, Ekwabi  Majungu kama malipo ya kiwanja kilichopo kijiji cha Ukuni wilayani Bagamoyo huku akionyesha yeye ni mmiliki, akijua ni uongo.

Kosa la saba, tarehe tofauti kama hiyo akiwa eneo la Upanga jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alijipatia Sh5 milioni kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa mtumishi wa Takukuru, Rose Shigela, kama malipo ya kiwanja kilichopo kijiji cha Ukuni wilayani Bagamoyo, huku akionyesha yeye ni mmiliki  akijua ni uongo.

Katika kosa la nane, kati ya tarehe tofauti Januari 2013 na Mei 2018 akiwa eneo la Upanga jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alijipatia Sh1.47 bilioni huku akijua fedha hizo ni zao la makosa mengine.