Kesi ya ‘Mpemba wa Magufuli’ mahakama yatoa siku saba

Muktasari:

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imetoa siku saba kwa upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Yusuf Ali maarufu kama ‘Mpemba wa Magufuli' na wenzake, kuja kueleza hatua waliyofikia katika shauri hilo, ili kesi hiyo iweze kuendelea.


Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imetoa siku saba kwa upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Yusuf Ali maarufu kama ‘Mpemba wa Magufuli' na wenzake, kuja kueleza hatua waliyofikia katika shauri hilo, ili kesi hiyo iweze  kuendelea.

Yusuf na wenzake  watano, wanakabiliwa na mashtaka manne, likiwemo la kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh785.6milioni.

Uamuzi huo umetolewa leo, April 2, 2019 na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, baada ya upande wa mashtaka kuomba wapewe siku chache ili waje kuieleza mahakama hatua walizofikia.

"Tumeshachoka na hizi taarifa zenu...nyie upande wa mashtaka mmekuwa na lugha za kujirudiarudia tuu kila mara...jambo ambalo linasababisha kucheleweshwa kwa kesi hii kusonga mbele," alisema Hakimu Simba.

Hakimu Simba alifafanua kuwa Februari 25, Machi 14 na Machi 25, mwaka huu, upande wa mashtaka walikuja na maelezo hayo hayo kuwa wanaomba tarehe fupi ili waje kuieleza mahakama hatua walizofikia, jambo ambalo halikubaliki.

"Sasa basi nataka upande wa mashtaka Aprili 9, mwaka huu, mje kutueleza mmefikia hatua gani siyo kurudia hizo lugha zenu... tunataka mtueleze mmefikia hatua gani...  hatuwezi kuendelea na lugha hizo kila siku," alisema Hakimu Simba.

Awali, Wakili wa Serikali, Elia Athanas, alidai shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kutajwa na kwamba Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi aliomba kupewa siku chache ili aje kutoa taarifa ya jalada la shauri hilo lilipofikia.

"Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi ameiomba Mahakama impe siku chache ili aje kuwasilisha taarifa ya jalada la shauri hilo lilipofikia kwa sababu leo ameshindwa kufika mahakamani kutokana na kuwa msibani," alidai Athanas.

Athanas baada ya kueleza hayo, wakili wa utetezi, Hassan Kiangio alidai wamechoshwa na maelezo ya upande wa mashtaka, hivyo wameomba mahakama iwasisitize ili kesi hiyo iweze kuendelea.

Hakimu Simba baada ya kusikiliza hoja za pande zote, aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 9, mwaka huu, itakapotajwa na washitakiwa walirudishwa rumande kutokana na kesi inayowakabili kutokuwa na dhamana.

Mbali na Yusuph, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Charles Mrutu, mkazi wa Mlimba, Morogoro, Benedict Kungwa, mkazi wa Mbagala Chamazi, Jumanne Chima, mkazi wa Mbezi, Ahmed Nyagongo ambaye ni dereva na Pius Kulagwa.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanadaiwa, katika tarehe tofauti kati ya Januari, 2014 na Oktoba, 2016 wakiwa Dar es Salaam, Tanga, Iringa na Mtwara, walijihusisha na mtandao wa ujangili kwa kukusanya na kuuza nyara za Serikali ambazo ni vipande 50 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Dola180,000 sawa na Sh392.8milioni bila kuwa na kibali cha mkurugenzi wa wanyamapori.

Pia wanadaiwa, Oktoba 26, 2016 wakiwa Mbagala Zakhem, walikutwa na vipande 10 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilo 13.85 vikiwa na thamani ya Dola30,000 (Sh 65.4milioni ).

Vile vile, Oktoba 27, 2016, wakiwa Tabata Kisukuru walikutwa na vipande vinne vya meno hayo vyenye uzito wa kilo 11.1 vikiwa na thamani ya Dola15,000 (Sh 32.7 milioni).

Wanadaiwa pia, Oktoba 29, 2016 walikutwa na vipande 36 vyenye thamani ya Sh294.6 milioni bila kuwa na kibali cha mkurugenzi wa wanyamapori.