Kesi ya Halima Mdee yakwama

Muktasari:

Kesi ya kutoa lugha chafu dhidi ya Rais John Magufuli inayomkabili mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee imekwama kusikilizwa katika  Mahakama  ya Hakimu Mkazi Kisutu kutokana na wakili wa Serikali kutokuwapo.

Dar es Salaam. Kesi ya kutoa lugha chafu dhidi ya Rais John Magufuli inayomkabili mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee imekwama kusikilizwa katika  Mahakama  ya Hakimu Mkazi Kisutu kutokana na wakili wa Serikali kutokuwapo.

Wakili wa Serikali, Daisy Makakala mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba ameeleza kesi hiyo ilipelekwa mahakamani hapo leo kuomba kuahirishwa kwa sababu zilizo nje ya uwezo wake.

“Tunaye shahidi ndugu, Abdi Chembeya lakini kwa leo hatutaweza kuendelea na kesi hii kutokana na sababu zilizopo nje ya uwezo wetu, tunaomba tarehe nyingine," ameomba Makakala.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Simba alitaka Mahakama ielezwe sababu za kesi hiyo kutoendelea wakati shahidi yupo.

Katika majibu yake, wakili Makakala ameeleza walikuwa waendelee lakini  wakili aliyekuwa akisimamia kesi hiyo tangu mwanzo hayupo.

Kwa upande wake, wakili wa utetezi, Hekima Mwasipu amesema bado miezi minne tu kesi hiyo itimize miaka miwili tangu ianze kusikilizwa na kuiomba Mahakama kuahirisha kesi hiyo kwa mara ya mwisho.

Hakimu Simba amesema sababu zilizotolewa ni za msingi na kuahirisha kesi hiyo na kupanga itaendelea tena Aprili 16 na 24.

Hadi sasa mashahidi watatu wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi katika kesi hiyo akiwamo mkuu wa kituo cha polisi cha Urafiki, mrakibu wa Polisi (SP) Batseba Kasanga.

Inadaiwa kuwa Julai 3, 2017 katika ofisi za makao makuu ya Chadema zilizopo mtaa wa Ufipa wilayani Kinondoni, Mdee alitamka maneno mabaya dhidi ya  Rais John Magufuli akisema: “Anaongea hovyo, anatakiwa  afungwe breki” kitendo kinachodaiwa kuwa ni kumdhalilisha Rais na kuhatarisha uvunjifu wa amani.

                  >>Sababu Halima Mdee kuitwa polisi hii hapa

                 >>Mdee ahojiwa kwa saa mbili, anyimwa dhamana

                >>Chadema yalaani polisi kumshikilia Halima Mdee