Kesi ya Seth, Rugemalira habari ni ile ile

Muktasari:

Upande wa mashtaka  katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mfanyabiashara Herbinder Seth na mwenzake James Rugemalira wameieleza mahakama ya hakimu mkazi Kisutu kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.


Dar es Salaam. Upande wa mashtaka  katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mfanyabiashara Herbinder Seth na mwenzake James Rugemalira wameieleza mahakama ya hakimu mkazi Kisutu kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi Februari 14, 2019 na wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai mbele ya hakimu mkazi mkuu, Huruma Shaidi  wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Shaidi  ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 28, 2019  kwa ajili ya kutajwa.

Washtakiwa hao wanasota rumande tangu Juni 19, 2017 walipofikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza, mara zote walizofikishwa mahakamani, inaelezwa kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika.

Wawili hao wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi  kwa kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kughushi nyaraka, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu,  kutakatisha fedha  na kuisababisha Serikali hasara ya dola 22.1milioni za Marekani na Sh309bilioni.

Washtakiwa hao wanadaiwa Oktoba 18, 2011 na Machi 19 , 2014 jijini Dar es Salaam walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ili kutenda kosa.

Aidha, inadaiwa katika mashitaka ya kujipatia fedha kwamba  kati ya  Novemba 28 na 29, 2011 na Januari 23,2014 katika makao makuu ya Benki ya Stanbic Kinondoni  na Benki ya Mkombozi tawi la Mtakatifu Joseph,  kwa ulaghai walijipatia kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dola 22.1 milioni za Marekani  na Sh309.4bilioni.

Pia washitakiwa wote wanadaiwa kuisababishia Serikali hasara, inadaiwa walitenda makosa hayo Novemba 29, 2013 katika Benki ya Stanbic tawi la  kati kinondoni, kwa vitendo vyao waliisababishia Serikali hasara ya Dola 22, 198, 544.60 za Marekani na Sh309bilioni.

Kati ya Novemba 29,2013 na Januari 23, 2014 maeneo tofauti Dar es Salaam kwa pamoja walitenda kosa la kutakatisha fedha kwa kuchukua fedha kutoka BoT ambazo ni dola 22.1 milioni za Marekani na Sh309.4  bilioni wakati wakijua fedha hizo ni zao la kujihusisha na genge la uhalifu.

Washitakiwa hao wapo rumande kwa kuwa mashtaka hayo hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.