Kesi ya Seth, Rugemalira yakwama tena

Muktasari:

  • Hakimu mfawidhi wa mahakama hiyo, Kelvin Mhina ameahirisha kesi hiyo leo hadi Agosti 30, 2018 baada ya wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai kueleza upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Dar es Salaam. Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mshtakiwa Habinder Seth na mwenzake, leo Alhamisi 16, 2018 imeahirishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu hadi Agosti 30, 2018.

Hakimu mfawidhi wa mahakama hiyo, Kelvin Mhina ameahirisha kesi hiyo leo hadi Agosti 30, 2018 baada ya wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai kueleza upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Swai ameomba kesi hiyo ipangiwe tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.

Hata hivyo, Hakimu Mhina amesema kesi hiyo imeahirishwa kwa kuwa hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi anayeiendesha  kesi hiyo anaumwa.

Mbali na Seth, mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni mfanyabiashara, James Rugemalira, ambao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 12, katika Mahakama hiyo.

Mashtaka hayo ni uhujumu uchumi kwa kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu, kuhushi, kutoa nyaraka za kughushi.

Pia wanadaiwa kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu na kutakatisha fedha.