Kesi ya Seth, Rugemarila habari ileile

Mkurugenzi wa VIP Engineering, James Rugemalira na Mwenyekiti Mtendaji wa IPTL, Harbinder Sing Sethi wakitoka katika chumba cha mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam jana. Picha  na Said Khamis

Muktasari:

Upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mfanyabiashara Herbinder Seth na James Rugemarila, umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika

Dar es Salaam. Upande wa Mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mfanyabiashara Herbinder Seth na mwenzake James Rugemarila, umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi Aprili 25, 2019 na wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaidi kesi hiyo ilipotajwa.

Swai amedai kuwa shauri hilo limekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi haujakamilika, hivyo kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Shaidi ameahirisha kesi hiyo hadi Mei 9, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Washtakiwa hao wanasota rumande kuanzia Juni 19, 2017 toka walipofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza kutokana na upelelezi wa kesi hiyo kutokamilika.

Seth na Rugemarila wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi kwa kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kughushi nyaraka, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha na kuisababisha Serikali hasara ya Dola 22.19 milioni za Marekani na Sh309.46 bilioni.

Washtakiwa hao wanadaiwa Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 jijini Dar es Salaam walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ili kutenda kosa.

Pia, inadaiwa katika mashtaka ya kujipatia fedha kwamba  kati ya Novemba 28 na 29, 2011 na Januari 23, 2014 katika makao makuu ya Benki ya Stanbic Kinondoni  na Benki ya Mkombozi tawi la Mtakatifu Joseph,  kwa ulaghai walijipatia kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dola 22.19 milioni za Marekani na Sh309.46 bilioni.

Pia, washtakiwa wote wanadaiwa kuisababishia Serikali hasara na inadaiwa walitenda makosa hayo Novemba 29, 2013 katika Benki ya Stanbic tawi la Kinondoni, kwa vitendo vyao waliisababishia Serikali hasara ya Dola 22.19 milioni na Sh309.46 bilioni.

Kati ya Novemba 29, 2013 na Januari 23, 2014 maeneo tofauti ya Dar es Salaam kwa pamoja walitenda kosa la kutakatisha fedha kutoka BoT ambazo ni Dola 22.19 milioni na Sh309.46 bilioni wakijua fedha hizo ni zao la kujihusisha na genge la uhalifu.

Washitakiwa hao wapo rumande kwa kuwa mashtaka hayo hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.