Kesi ya mabosi Jamii Forum yakwama

Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe (kushoto) akizungumza na Mkurugenzi wa Jamii Media Max Mero katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Kesi inayomkabili Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jamii Forum, Maxence Melo na mwenzake, Micke William imeshindwa kuendelea baada ya wakili wa Serikali kuomba muda wakupitia jalada la shauri hilo.

Dar es salaam. Kesi ya kuzuia jeshi la polisi kufanya uchunguzi inayomkabili Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jamii Forums, Maxence Melo na mwenzake, Micke William imeshindwa kuendelea na utetezi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Wakili wa Serikali, Sylvia Mitanto amedai leo Mei 16 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa, shauri hilo lilikwenda mahakamani hapo kwa ajili ya utetezi lakini ndiyo amekabidhiwa jalada hivyo kuomba muda kwa ajili ya kulipitia.

"Shauri hili limekuja kwa ajili ya utetezi, muda mfupi uliopita ndio nimekabidhiwa jalada hivyo naomba ahirisho fupi niweze kulipitia jalada" ameomba Wakili Mitanto.

Kwa upande wake, Hakimu Simba alieleza kuwa, wakili aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo amehama na kuutaka upande wa mashtaka  ujitahidi ili tarehe itakayopangwa isikilizwe utetezi wa washtakiwa wote ili imalizike kabla ya mwezi wa sita.

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 3 mwaka huu kwa ajili ya upande wa utetezi kupeleka  mashahidi.

Tayari mashahidi wanne wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi wao dhidi ya washtakiwa hao na Mahakama kuwakuta na kesi ya kujibu.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanadaiwa kuzuia Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi kinyume cha Sheria namba 22 (2) cha Sheria ya Makosa ya Mtandano Namba 14 ya mwaka 2015.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo kati ya Aprili Mosi, 2016 na Desemba 13, 2016  katika maeneo ya Mikocheni wilayani Kinondoni.