Kiemi - msomi anayetengeneza mamilioni kwenye ufugaji nyuki

Muktasari:

Waswahili wanasema ukitaka masisha bora kwa familia yako anzisha biashara na kamwe usitegemee wadhfa ulionao au elimu yako kwani huwezi kuwarithisha watoto wako.

Waswahili wanasema ukitaka masisha bora kwa familia yako anzisha biashara na kamwe usitegemee wadhfa ulionao au elimu yako kwani huwezi kuwarithisha watoto wako.

Hili linajidhihirisha kwa watu wengi waliofanikiwa kiuchumi bila kujali wanafahamika au hawajulikani. Miongoni mwa watu hao ni Philemon Kiemi (31), mhitimu wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA) mwaka 2012 tofauti na wenzake waliobahatika kuajiriwa ofisi tofauti.

Kiemi alianza ufugaji tangu mwaka 2008 akiwa kidato cha tano akijifunza kutoka kwa baba yake aliyekuwa na mizinga 45 mwaka huo akiendesha shughuli zake katika Kijiji cha Kisaki mkoani Singida.

Licha ya mizinga hiyo, Kiemi alirithi ekari 200 kutoka kwa baba yake na ili kuimarisha ufugaji wake, alianzisha chama cha ushirika alichokiita Singida Youth Entrepreneur Consultant and Cooperative Society (SYECCOS) mwaka 2008 akishirikiana na kaka yake, Joseph Kiemi.

Katika shamba ambalo awali lilikuwa na mizinga michache ya baba yake, Kiemi anasema alianza kufuga kuku ambao walimwezesha kutengeneza mizinga 150 ambayo sasa imefika 8,000.

“Baada ya kuingia kwenye sekta hii nilianza kutengeneza mizinga. Licha ya kuendelea na ufugaji nafundisha wajasiriamali wengine, napokea watalii wa nyuki na kuotesha miche ya miti ninayoiuza kwa wafugaji wenye mahitaji nayo,” anasema Kiemi.

Kutokana na juhudi alizoweka, alikuwa anaongeza eneo la ufugaji taratibu na mpaka sasa ana takriban ekari 40,000 zilizo maeneo tofauti. Kikiitwa Kijiji cha Nyuki, Kiemi anasema anazo ekari 7,000 zenye mizinga 3,000 zinazohudumiwa na wafanyakazi 80 zilipo ofisi zake.

Vilevile, ana ekari 32,000 katika eneo liitwalo Jiji la Nyuki ambako ameajiri wafanyakazi 172. Ingawa amekuwa akiwekeza fedha anazopata kutokana na shughuli zake, Kiemi anaamini yeye ndiyo mfugaji mkubwa wa nyuki nchini.

“Mwaka 2017, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alinipa tuzo ya mshindi wa chama bora cha ushirika nchini kwa sababu uwekezaji wangu ulifika Sh1.7 bilioni bila kukopa sehemu yoyote,” anasema.

Utalii wa nyuki

Mbali na fedha anazoingiza kwenye asali, Kiemi anasema biashara ya mizinga inaweza kuingiza mpaka Sh200 milioni kwa mwaka biashara ikienda vizuri. Vilevile, anatoa mafunzo ya ufugaji wa nyuki na kila mwezi hupata mpaka wanafunzi 100.

Wahitimu waliotoka hapa wameajiriwa katika mashamba mengine ya nyuki. Tunapokea watalii pia. Mtu anakuja akiamini Mungu alisema tutakula maziwa na asali kwa hiyo anataka awaone nyuki na asali iliyolinwa,” anasema.

Wakati Wakristo wakiwahusisha nyuki na dini yao, baadhi ya watalii, anasema wanaenda kujifunza uchongaji wa mizinga, mafunzo yanayotolewa zaidi kwa vitendo. Wanafunzi hujifunza kuchonga na kuhudumia mizinga pamoja na kupanda miti kwa ajili ya kuipachika.

Kwa mafanikio madogo aliyonayo, Kiemi anasema yalichochewa na mafunzo ya miezi sita aliyoyapata nchini Israel muda mfupi baada ya kuhitimu SUA ambako kulikuwa na utaratibu wa kupeleka wanafunzi wake mashariki ya kati.

Baada ya safari hiyo iliyomtoa nje ya mipaka ya nchi, anasema milango ilifunguka na hizi sasa anapata mialiko mingi ya kimataifa ambayo humpa nafasi ya kubadilishana uzoefu na wafugaji wengine wa nyuki.

Akiitaja michache, Kiemi anasema mwaka 2013 alihudhuria mkutano nchini Ukraine na miaka miwili baadaye (2015) akaenda Korea Kusini mwaka 2015 kabla haalikwa Uturuki mwaka 2017 alikowasilisha mada kwa dakika 20. Agosti mwaka huu ataenda Canada kwenye mkutano wa 46 wa wafuga nyuki duniani.

Akiwa na mtambo wenye uwezo wa kusindika tani tani moja ya asali kwa saa moja ambayo nyingi huiza soko la ndani, Kiemi anasema anaendelea kuongeza uwekezaji ili kuzalisha asali nyingi zaidi.

“Nina ndoto ya kuzalisha asali nyingi zaidi ikiwezekana iwe sawa na uzalishaji wa Tanzania wa tani 38,000. Tunavyozungumza nazalisha tani 38 kila mwaka ingawa mwaka huu naweza kufikisha tani 100 kwa sababu tumeongeza mizinga na hatujavuna bado,” anasema Kiemi.

Mafunzo

Kwenye kitabu chake kilichochapishwa mwaka 1926 alichokiita ‘The Richest Man in Babylon,’ George Clason anasisitiza umuhimu wa watu waliofanikiwa kuzungumza na watu wa kawaida wasio na maarifa juuya sekta walizomo.

Clason anapendekeza wajasiriamali wadogo kukaa na mabilionea ili wafundishwe mbinu za kuzitumia fursa zinazowazunguka kujitegemea kiuchumi. Kwa mfumo huo, mwandishi huyo anasema Taifa litakuwa na mabilionea wengi.

Mmoja wa wanaoitumia falsafa hiyo ni Kiemi ambaye anatumi amuda wake kuwaandaa wafugaji wengine wa nyuki kwa kuwaongezea maarifa na mbinu za kuepuka kuanguka.

Miongoni mwa wahitimu wa mafunzo yanayotolewa a Kiemi ni Saada Fadhili kutoka Mburahati jijini Dar es Salaam aliyeenda Singida kusaka ujuzi wa kufuga nyuki.

“Nimekuja kujifunza baada ya kusoma blogu ya kampuni, nikawasiliana nao. Nataka nianzishe mradi wangu hapa hapa Singida kwa kuwa bado kuna maeneo makubwa,” anasema Saada ambaye kwa sasa ameajiriwa katika kampuni hiyo ili kuimarisha zaidi uelewa wake kuhusu ufugaji huo.

Ufugaji nyuki

Ufugaji nyuki nchini hufanyika kwa ajili ya kujiingizia kipato au kulinda mazingira ambayo husaidia kustahimilisha hali ya hewa. Uvunaji holela wa misitu husababisha mabadiliko ya hai ya hewa inayochangia mmonyoko wa udongo, ukame au mafuriko hivyo kuathiri shughuli za wakulima na nyinginezo.

Kwa uzalishaji wa tani 38,000 kwa mwaka, Tanzania inatajwa kuwa nchi ya pili duniani kwa uzalishaji wa asali ikichuana na Ethiopia inayozalisha tani 50,000. Kati ya kiasi hicho, takwimu zinaonyesha Tanzania inasafirisha asilimia 10 ya asali nje ya nchi na inayobaki inatumika nchini.

Nchi zinazohitaji asali ya Tanzania kwa wingi ni Afrika Kusini, India, Botswana, Namibia, Canada, Dubai, Kuwait, Irak, Iran, Japan, China na Lebanon.

Nyingine ni Saudi Arabia, Oman Rwanda, Uganda, Kenya, Ufaransa, Uholanzi, Norway, Ujerumani na Uingereza, Marekani na Ireland.

Kwa wastani, pato linalotokana na nta kwa mwaka ni Sh2.6 bilioni wakati asali ikichangia Sh818.4 milioni ambalo linaweza kuongezeka kama uzalishaji utaimarishwa.