Kifungu kilichotumika kuwaachia huru polisi wanane hiki hapa

Muktasari:

Kifungu 91(1) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai sura ya 20 na marekebisho ya mwaka 2002 ndio kimetumika kuachiwa huru askari polisi wanane waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya kusafirisha kilo 319 za dhahabu na Sh305 milioni

Mwanza. Kifungu 91(1) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai sura ya 20 na marekebisho ya mwaka 2002 ndio kimetumika kuachiwa huru askari polisi wanane waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya kusafirisha kilo 319 za dhahabu na Sh305 milioni.

Mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza leo Alhamisi Julai 18, 2019, wakili wa Serikali mkuu, Castus Ndamugoba ametumia kifungu hicho kuieleza mahakama hiyo kuwa ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka nchini (DPP) haina haja ya kuendelea na shauri hilo.

Kutokana na ombi hilo la Jamhuri, Hakimu Mkazi mfawidhi Mkoa wa Mwanza, Rhoda Ngimilanga aliyekuwa akisikiliza shauri hilo namba 1/2019 aliifuta na kuwaachia huru washtakiwa ambao kwa pamoja waliondoka mahakamani wakitumia gari moja aina ya Toyota Land Cruiser nyeupe.

Kinavyosema kifungu cha 91(1) na 91(2)

“Katika kesi yoyote ya jinai na katika hatua yoyote ile kabla ya hukumu au uamuzi, kama itakavyokuwa, Mkurugenzi wa Mashtaka anaweza kuweka nolle prosequi, aidha kwa kueleza mahakamani au kwa kuiambia mahakama husika kwa maandishi kwa niaba ya Jamhuri kuwa mwenendo hautaendelea.”

“Na baada ya hapo mtuhumiwa ataachiwa mara moja kuhusiana na shtaka ambalo nolle prosequi imewekwa na kama amepelekwa gerezani atatakiwa kuachiwa, au kama yuko chini ya dhamana wadhamini wake watakoma kuwa wadhamini,” kinaeleza kifungu hicho.

Hata hivyo, kifungu hicho kinatoa fursa ya mshtakiwa anayeachiwa kuweza kukamatwa na kufunguliwa upya mashtaka.

“Lakini kuachiwa huko kwa mtuhumiwa hakutachukuliwa kama kizuizi kwa mashtaka mengine ya baadaye dhidi yake kwa kutumia maelezo hayo hayo,” kinasema sehemu ya kifungu hicho cha 91(1).

Kifungu cha 91(2) kinasema; “Iwapo mtuhumiwa hayupo mbele ya mahakama wakati nolle prosequi inawekwa, msajili au karani wa mahakama atatakiwa mara moja kuhakikisha notisi ya maandishi ya kuwekwa kwa nolle prosequi inapelekwa kwa mtunzaji wa gereza ambamo mtuhumiwa anaweza kuwa anazuiwa.”

“Na kama mtuhumiwa amepelekwa kwa kusikiliza shauri, kwa mahakama ya chini ambako ndiko alikosikilizwa na mahakama hiyo italazimika mara moja kuhakikisha notisi kama hiyo ya maandishi anapewa shahidi yeyote anayewajibika kutoa ushahidi na kwa wadhamini wake (kama wapo) na vilevile kwa mtuhumiwa na wadhamini wake kama alishatolewa kwa dhamana.”

Walivyokamatwa na kushtakiwa

Askari hao pamoja na wafanyabiashara wanne wa dhahabu walikamatwa Januari 5, 2019 wilayani Sengerema na kufikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Januari 11, 2019 wakikabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi, kupanga na kula njama ya kutenda kosa, kutakatisha fedha na rushwa.

Wafanyabiashara wanne wa dhahabu, Hassan Sadiq, Emmanuel Mtemi, Kisabo Nkinda na Sajid Hassan waliostakiwa pamoja na askari hao walikiri mashtaka dhidi yao na kuhukumiwa vifungo kati ya miaka mitano hadi 15 au faini kati ya Sh5 milioni hadi Sh100 milioni.

Wafanyabiashara hao walilipa zaidi ya Sh529.8 milioni kukwepa kwenda jela.