Kigogo Jamii Forum, mwenzake wana kesi ya kujibu

Muktasari:

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewakuta na kesi ya kujibu mkurugenzi mtendaji wa mtandao wa Jamii Forum, Maxence Melo (40) na mwenzake, Micke William Mushi

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu  imewakuta na kesi ya kujibu mkurugenzi mtendaji wa mtandao wa Jamii Forum, Maxence Melo (40) na mwenzake, Micke William Mushi.

Uamuzi huo umetolewa leo Ijumaa Februari 22, 2019 na Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Thomas Simba, baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi watatu na kielelezo kimoja.

Kabla ya kutolewa uamuzi huo wakili wa Serikali, Elia Athanas amedai mahakamani hapo kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya uamuzi kama washtakiwa hao wana kesi ya kujibu au la.

"Washtakiwa wote wapo mbele ya mahakama yako na upande wa mashtaka tupo tayari kwa ajili ya uamuzi" amedai Athanas.

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Simba aliwasomea uamuzi huo akibainisha kuwa washtakiwa wanakabiliwa na shtaka moja la kuzuia Jeshi la Polisi kufanya upelelezi katika kesi ya jinai namba 456/2016.

Hakimu Simba amesema upande wa mashtaka walileta mashahidi watatu na kielelezo kimoja kuthibitisha mashtaka yao.

"Baada ya mahakama kupitia ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka, mahakama hii imeona kuwa washtakiwa wote wana kesi ya kujibu, hivyo wanatakiwa kujitetea,” amesema Hakimu Simba.

Simba amesema washtakiwa hao wanaweza kujitetea kwa njia ya kiapo au bila kuapa au kukaa kimya ili mahakama iamue.

Baada ya kueleza hayo, wakili anayewatetea washtakiwa hao, Nashon Mkungu amedai kuwa wateja wake watajitetea kwa kiapo na wanatarajia kuwa na mashahidi watano.

"Upande wa utetezi tunatarajia kuleta mashahidi watano, hivyo tunaomba tarehe ya kuanza kujitetea" amedai wakili Mkungu.

Wakili wa utetezi baada ya kueleza hayo, Hakimu Simba amepanga Machi 14 na 19, 2019 washtakiwa hao waanze kujitetea.

"Washtakiwa wataanza kujitetea Machi 14 na 19, hivyo nataka upande wa utetezi mje na mashahidi hao kwa muda tuliopanga ili kesi hii iweze kuisha mapema kabla mwezi Machi haujaisha" alisema Simba.

Hata hivyo, uamuzi huo umefikiwa baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wao wa mashahidi watatu waliotoa ushahidi dhidi ya washtakiwa hao.

Miongoni mwa mashahidi waliotoa ushahidi katika kesi hiyo ni Ofisa Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SSP Ramadhan Kindai, ambaye aliieleza mahakama hiyo kuwa yeye ndiyo aliyetoa amri ya kukamatwa kwa Melo na Mushi baada ya kushindwa kutoa taarifa sahihi kuhusu habari iliyochapishwa kwenye mtandao wa JamiiForum.

SSP Kindai amedai kuwa waliomba kampuni hiyo taarifa kutokana na shauri lililofunguliwa na Usama Mohammed ambapo walihitaji kufanya uchunguzi wa kina kuhusu taarifa zilizochapishwa kwenye mtandao huo.

Shahidi huyo amedai Februari 19, 2016, mteja wao Mohammed ambaye ni ofisa msimamizi wa mauzo ya rejareja kutoka Kampuni ya Oil com, alifika ofisi ya mkuu wa upelelezi na kutoa malalamiko kwamba Februari 13, 2016, alisoma kwenye mtandao wa Jamii Forum ambapo ilidaiwa kampuni kampuni hiyo imekwepa kodi bandarini na wanaiibia Serikali.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa kuzuia Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi, kinyume na sheria namba 22 (2) ya Sheria ya Makosa ya Mtandano Namba 14 ya mwaka 2015.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo, kati ya Aprili Mosi, 2016 na Desemba 13, 2016 katika maeneo ya Mikocheni wilayani Kinondoni.