Kigoma, Kagera vinara wa kuchafua noti

Muktasari:

Mikoa ya Kigoma na Kagera imetajwa kuongoza kwa kuchafua na kuchakaza fedha tofauti na maeneo mengine Tanzania.

 



Kigoma. Wakazi wa mkoa wa Kigoma wametajwa kuongoza kwa uchafuzi wa fedha hususan noti kuliko mikoa yote nchini, wakifuatiwa na Kagera.

Kauli hiyo imetolewa leo na meneja msaidizi wa uhusiano wa umma kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Victoria Msina  alipozungumza na viongozi wa Serikali, madiwani, wafanyabiashara na baadhi ya wananchi mjini Kigoma.

"Utafiti tuliofanya tumebaini mkoa wa Kigoma unaongoza kwa kuchafua noti, fedha zinachakaa mno ukilinganisha na mikoa mingine ndiyo maana tumeamua kutoa elimu kwa umma tukianza na mikoa hii miwili (Kigoma na Kagera)," amesema Msina.

BoT wanalenga kufundisha watu wajue umuhimu wa kutunza fedha na kuepuka uchakavu wa noti na sarafu, sambamba na alama muhimu ili kutofautisha noti halali na bandia.

Meneja msaidizi wa utunzaji fedha na usalama kutoka BoT, Abdul Dollah ametaja baadhi ya sababu zinazofanya noti kuchakaa haraka ni utunzaji mbovu kama vile kushika pesa mikono ikiwa michafu.

"Kuna watu wanafanya kazi ya kuuza mkaa, samaki na mama lishe ambao kuna wakati hulazimika kupokea fedha mikono yao ikiwa michafu, matokeo yake fedha zinachakaa haraka," amesema Dollar.

Ili kuepuka noti kuchakaa mapema, ameshauri wananchi kufungua akaunti benki na kufanya malipo ya bidhaa kwa njia za kibenki au simu za mkononi.

Diwani wa Kigoma mjini, Hussein Kalyango amekiri noti nyingi zinazotumika Kigoma zimechakaa na ni vigumu kuzitumia unapofika mikoa mingine.

"Kuna noti tunazitumia hapa Kigoma lakini hizohizo ukifika nazo Dar es Salaam utaambiwa ni mbovu na hawazipokei. Kwa hiyo lazima BoT mtoe elimu hasa kwa jamii ili wajue umuhimu wa kutunza noti zisichakae mapema," amesema Kalyango.

Watumishi wa BoT wapo mkoani Kigoma kwa ziara ya siku tano kuelimisha jamii juu ya utunzaji bora wa noti na kuepuka uchakavu na wilaya za Uvinza na Kasulu.