Kigoma kupata umeme wa uhakika mwaka 2020

Friday July 12 2019

By Happiness Tesha, Mwananchi [email protected]

Kasulu.  Serikali ya Tanzania imejipanga ifikapo mwaka 2020 kuondokana na uzalishaji umeme kwa kutumia mafuta mkoani Kigoma.

Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa Julai 12, 2019 na naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu aliyepo kwenye ziara mkoani humo.

Amesema  katika kutimiza dhamira hiyo tayari ujenzi wa msongo wa umeme 132 KV kutoka wilayani Urambo mkoani Tabora hadi Kigoma umeanza na fedha kwa ajili ya kukamilisha kazi hiyo ipo.

Amesema lengo ni kuwa na umeme wa uhakika wa kukidhi mahitaji ya wananchi wa Mkoa huo na kwamba unaozalishwa sasa kwa kutumia mafuta hautoshelezi mahitaji wala kupunguza gharama za uendeshaji.

"Mkoa wa Kigoma ni moja ya mikoa ya kimkakati katika suala  zima la uanzishaji wa viwanda. Niwaombe wananchi kuchangamkia fursa hiyo na Serikali imeendelea kupunguza gharama za umeme," amesema Mgalu.

Mkuu wa wilaya ya Kasulu,  Simon Annange amesema Wilaya hiyo ni moja kati ya wilaya zenye shughuli nyingi za kiuchumi kutokana na kupakana na Burundi.

Advertisement

Advertisement