Kiingereza kuendelea kuwa lugha ya kufundishia nchini Tanzania

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako akijibu maswali bungeni katika kikao cha 44 cha mkutano wa Bunge la Bajeti, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Licha ya Kiswahili kupigiwa debe kuwa lugha ya kufundishia nchini Tanzania, Serikali imesisitiza Kiingereza kuwa lugha ya kufundishia kwa sababu ya umuhimu wake kitaifa, kikanda na kimataifa kwa mawasiliano na biashara ili kuwajengea wanafunzi ufahamu na umahiri wa lugha hiyo.


Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema Kiingereza kitaendelea kuwa lugha ya kufundishia na kujifunzia katika ngazi ya elimu ya sekondari, vyuo vya kati na vyuo vikuu.

Akijibu swali la mbunge wa Tabora Kaskazini (CCM), Almasi Maige leo Jumatano Juni 12, 2019, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amesema Kiingereza kitaendelea kutumika kwa sababu ya umuhimu wake kitaifa, kikanda na kimataifa kwa mawasiliano na biashara ili kuwajengea wanafunzi ufahamu na umahiri wa lugha hiyo.

Katika swali lake la msingi, Maige alitaka kujua ni lini Serikali itaanza kutumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia katika Shule za Msingi na Upili ili kukuza uelewa wa wanafunzi katika masomo yao, kuhoji ilipoishia nia ya Serikali kutumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia.

“Suala la matumizi ya lugha ya kufundishia na kujifunzia ni la kisheria kama ambavyo sheria ya elimu sura 353 inavyoelekeza. Sheria hiyo inabainisha matumizi ya lugha mbili za kufundishia na kujifunzia ambazo ni Kiswahili na Kiingereza.”

“Kwa sasa Kiswahili kinatumika kufundishia katika ngazi ya elimu ya awali na msingi, vyuo vya ualimu ngazi ya cheti na vyuo vya ufundi stadi,” amesema Profesa Ndalichako.