Kikwete ataja alichozungumza na Mengi kabla ya kifo chake

Muktasari:

  • Rais mstaafu, Jakaya Kikwete amesema kifo cha mwenyekiti mtendaji wa kampuni za IPP, Reginald Mengi ni pigo kwa kuwa taifa kwani limepoteza raia makini, mchapakazi na mzalendo

Dar es Salaam. Rais mstaafu, Jakaya Kikwete amesema kifo cha mwenyekiti mtendaji wa kampuni za IPP, Reginald Mengi ni pigo kubwa kwa taifa kwani limepoteza raia makini, mchapakazi na mzalendo.

Kikwete ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Mei 4  wakati akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kusaini kitabu cha maombolezo nyumbani kwa Mengi Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Amesema marehemu Mengi alikuwa ni mtu mwenye huruma na moyo wa kusaidia watu mbalimbali na ametumia utajiri wake kuwasaidia Watanzania wengi.

"Nilishtushwa na taarifa za kifo chake, si rahisi kuzungumza kutokana na hali ya majonzi. Nilikuwa Benin katika mkutano wenye ajenda ya kutokomeza malaria ndipo nilipopata taarifa hizi.”

"Kabla ya umauti kumkuta nilizungumza na kusalimiana naye kwa sababu alikuwa kama kaka yangu. Nilikubaliana naye kwamba nikirudi safari tutakutana na kuzungumza, kifo chake kimenishtua sana," amesema.

Kikwete amesema taifa lilitamani kuendelea na Mengi lakini Mungu ameshapitisha uamuzi wake na kilichobaki ni familia kuwa na moyo wa subira.

“Nimezungumza na mtoto wa Mengi aitwaye Abdiel nikamwambia yale aliyoyafanya Mengi yadumishwe na watoto ili bendera ya IPP iendelee kupepea,” amesema rais huyo mstaafu wa awamu ya nne.

Aidha, Kikwete amesema ni wakati wa Watanzania kuwaombea watoto na familia ya Mengi ili wayasimamie kwa ufanisi yalioachwa na mpendwa wao.

"Na sisi Watanzania tuwe watulivu tuache uongo wa kutunga mambo badala yake tusubiri watoto wake walioko naye watuambie ukweli. Mnayoyasema yaacheni subirini wanaye watakaporudi watatueleza ukweli," amesema Kikwete.