Kikwete ataja changamoto za demokrasia Afrika

Muktasari:

Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete amesema licha ya Umoja wa Afrika (AU) kufanikiwa katika malengo yake ya kuleta uhuru kwa nchi wanachama, bado kuna changamoto kubwa tatu ikiwamo kukosekana kwa utawala bora, umasikini na magonjwa.

Dar es Salaam. Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete amesema licha ya Umoja wa Afrika (AU) kufanikiwa katika malengo yake ya kuleta uhuru kwa nchi wanachama, bado kuna changamoto kubwa tatu ikiwamo kukosekana kwa utawala bora, umasikini na magonjwa.

Akizungumza katika tamasha la 11 la kitaaluma la Mwalimu JK Nyerere lililofanyika jana Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais Kikwete ambaye alikuwa mhadhiri wa heshima wa kongamano hilo alisema licha ya kuwepo kwa juhudi chanya za viongozi wa Afrika kuonyesha ubunifu wa mipango ya maendeleo, bado kuna tatizo la utawala.

“Kumekuwa na changamoto zinazohitaji kuangaliwa ambazo ni kuwepo kwa sheria kandamizi, ushiriki usioridhisha wa wananchi, kutokuwepo kwa uhuru wa habari na kutokuwepo kwa mikakati ya kupambana na rushwa,” alisema Kikwete.

Alisema kwa mujibu wa utafiti wa hivi karibuni kuhusu utawala, japo katika nchi za Afrika zimeonyesha kuridhisha kati ya mwaka 2018 hadi sasa, eneo la uchumi na jamii, utawala wa uchumi utendaji wa chini umeonekana katika eneo la demokrasia na utawala wa kisiasa.

“Kama watu wa Afrika hatuna njia nyingine bali kutatua hizi changamoto za utawala kama zilivyoelekezwa,” alisema.

Kikwete, ambaye amewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje alitumia muda mwingi wa hotuba yake kueleza historia ya mapambano ya ukombozi wa Afrika, na kusema kumekuwa na mikakati ya kuendelea kuikomboa Afrika kiutawala bora, ikiwa pamoja na mpango wa kujitathmini kiutawala bora (APRM).

Alisema “sina uhakika kama viongozi wa Afrika walikuwa wakisikiliza maoni ya wengine kuhusu utawala bora.

“Viongozi wetu wanatakiwa wachukue juhudi zote na mipango mikakati ambayo itatetea utekelezaji wa demokrasia na ushiriki wa wananchi katika masuala ya Umoja wa Afrika na utawala bora.”

Mbali na utawala bora, Kikwete alisema bara la Afrika bado linatawaliwa na umasikini na kwamba kati ya nchi 27 maskini zaidi duniani, 25 zipo Afrika.

Alisema kuna mikakati mbalimbali imefanywa ikiwa pamoja na kuanzishwa kwa mpango mpya wa ushirikiano wa kiuchumi (Nepad).

Mbali na umaskini, alisema bara la Afrika bado linakabiliwa na magonjwa na aliutaja ugonjwa wa malaria kuwa tishio zaidi.

Wakizungumza katika mjadala wa uhusiano kati ya dola na soko, mfanyabiashara maarufu nchini, Ally Mufuruki alikosoa wanasiasa wanaomtumia Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kupiga siasa ikiwa pamoja na kulaumu vyombo vya fedha vya kimataifa ikiwemo Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Mufuruki alisema kuna watu wanaomtumia Mwalimu Nyerere wakijifanya kupinga mabeberu wakati mwenyewe alishabadilisha mtazamo kabla hajafariki duniani.

“Nimesema makusudi kwasababu Mwalimu mara nyingi anatumika kama kisingizio cha kuendeleza siasa ambazo zilishashindwa za mwaka 1967, siasa ambazo mwenyewe alisema zimeshindwa,” alisema Mufuruki.

“Wapo vijana wengine ambao hata hawakuwepo wakati Mwalimu akiwa serikalini, lakini utawakuta wakisema ‘kama Mwalimu alivyosema’, si kweli kwasababu alishabadili mtazamo. Mwalimu alikuwa na akili na mtu mwenye akili lazima akubali kubadilika.”

Alisema kama Mwalimu Nyerere angekuwepo angetaka tujadili athari za siasa zake kwa uwazi.

“Hata kama ingekuwa ni kum-criticize (kumkosoa), Mwalimu alikuwa intellectual (msomi), haogopi kuwa criticized, intellectual haogopi kusema kuwa amekosea.”

Mufuruki ambaye pia ni mwenyekiti wa bodi ya Kampuni ya Vodacom amelitetea Shirika la Fedha la Kimataifa na Benki ya Dunia kuwa hayahusiki na umasikini wa nchi zinazoendelea.

“Wasomi wamekuwa wakisema matatizo tuliyonayo katika kuendesha nchi yametokana na sera mbovu za IMF na WB, wanasema sera za kibeberu.

“Inaweza kuwa kweli, lakini tusiishie hapo. Mimi nakataa kwa sababu IMF kazi yao ni kusaidia kukwamua nchi zilizokwama na madeni,” alisema.

Alisema mpaka mwaka 1980 Tanzania haikuwa na shida ya kusaidiwa na IMF na WB, lakini uchumi uliporomoka kwa kasi na ikafika mahali nchi ikaomba WB na IMF waje kusaidia kupanga uchumi.

“Sasa kama walitushauri kwamba mbinafsishe viwanda, Serikali iache kufanya hivi, na sisi tukatekeleza, kwa nini tulaumu?” alihoji.

Mbali na Mufuruki, wanajopo wengine walioshiriki walikuwa pamoja na Dk Suzan Kavuma kutokana Chuo Kikuu cha Makerere Uganda aliyezungumzia haja ya wawekezaji wa ndani kulindwa.

Pia alikuwepo mtafiti mwandamizi kutoka taasisi ya utafiti wa kuondoa umasikini, Dk Blandina Kilama.