Kikwete atembelea eneo litakapojengwa tawi la UDSM jijini Mbeya

Muktasari:

  • Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Rais mstaafu Jakaya Kikwete amewasili jijini Mbeya leo Jumanne na kutembelea eneo kitapojengwa chuo kishiriki cha UDSM.

Mbeya. Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Jakaya Kikwete leo Jumanne Machi 26, 2019 ametembelea eneo litakalojengwa tawi la chuo hicho eneo la Tanganyika Parkes jijini Mbeya.

Kikwete ambaye ni Rais mstaafu amesema wanatarajia kujenga chuo cha afya na sayansi shirikishi ili kuongeza idadi ya wanafunzi wanaotaka kusoma masomo hayo. Eneo hilo lipo kilomita 20 kutoka Mbeya mjini likiwa na ukubwa wa ekari 3,000

Licha ya tawi hilo kuanza kufanya kazi Desemba mwaka 2017, wanakabiliwa na uhaba wa vyumba vya kufundishia na malazi kwa ajili ya wanafunzi 1,146 na watumishi 85 waliopo.

“Mpaka sasa tunatumia majengo ya kuazima kutoka Hospitali ya Rufaa Mbeya na chuo cha Teofilo Kisanji, hii ni changamoto ambayo inatakiwa tuishughulikie mapema. Naomba Serikali itupe ruhusa ya kujenga eneo lililotengwa na tupo tayari kuwalipa fidia wananchi wanaofanya shughuli za kilimo eneo hilo,” amesema Kikwete.

Kikwete amesema wana matarajio ya kutoa madaktari wenye sifa na viwango watakaopambana na soko la ajira popote duniani na bahati nzuri UDSM ina sifa ya kutoa wanafunzi bora kuliko vyuo vingine.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amesema uwepo wa chuo hicho umepunguza malalamiko ya wananchi kuhusu uhaba wa madaktari katika Hospitali ya Rufaa Mbeya kwa sababu wahadhiri wanaofundisha chuoni hapo wanatoa huduma hospitalini hapo pia.