Kikwete ateua wakuu wa mikoa wapya

Tuesday September 15 2015

Mwantumu Mahiza: Amehama kutoka Lindi kwenda

Mwantumu Mahiza: Amehama kutoka Lindi kwenda Tanga 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Dar es Salaam. Baada ya kuangushwa kwenye kura za maoni ndani ya CCM, Jimbo la Mvomero, Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, wadhifa alioanza kuutumikia Jumamosi iliyopita.

Makalla amechukua nafasi ya Leonidas Gama ambaye anawania ubunge wa Songea. Taarifa ya Ikulu imesema, Rais Jakaya Kikwete amefanya uteuzi wa wakuu wa mikoa wawili huku akiwabadilishia vituo vya kazi wengine wawili.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema katika taarifa hiyo kuwa wakati Makalla akienda Kilimanjaro, Jordan Rugimbana, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro anakwenda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi. Pia Rais amejaza nafasi ya Stella Manyanya mkoani Rukwa, anayegombea ubunge Jimbo la Nyasa.

Makamishana wa NEC

Rais Kikwete pia amewateua makamishna wawili wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Walioteuliwa na Mary Longway na Asina Omari na uteuzi wao ulianza jana. Longway ni Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Asina Omari ni Wakili wa Kujitegemea.

Naibu AG

Katika hatua nyingine, Rais Kikwete amemteua Dk Tulia Ackson kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali (NAG) kuanzia Jumatano, Septemba 9, mwaka huu. Kabla ya uteuzi wake, Dk Ackson alikuwa Mhadhiri wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

CEO NDC

Wakati huo huo, Rais Kikwete amemteua Mlingi Mkucha kuwa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) kuanzia Septemba 9, mwaka huu, 2015. Mkucha ambaye ni mwanasheria na mwajiriwa wa NDC kwa miaka 14 iliyopita, anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Gideon Nassari aliyestaafu kwa mujibu wa sheria.

Mganga Mkuu wa Serikali

Rais Kikwete amemteua Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tiba na Afya Shirikishi cha Muhimbili, Dar es Salaam, Profesa Muhammed Kambi kuwa Mganga Mkuu wa Serikali kuanzia Septemba 9, 2015.

Advertisement