Kikwete autaja uzalendo, uchapakazi wa Mengi

Rais msta-afu, Jakaya Kikwete aki-saini kitabu cha maom-bolezo ya Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi ali-pokwenda kuifariji na kutoa pole kwa familia ya mare-hemu Mengi, jijini Dar es Salaam jana. Picha na Said Khamis

 

Dar/Hai. Rais mstaafu Jakaya Kikwete amesema kifo cha Reginald Mengi ni pigo kwa Taifa ambalo limempoteza raia makini, mchapakazi na mzalendo huku akiwataka watu wanaotunga uongo kuhusu kifo cha mwenyekiti huyo wa Kampuni za IPP, kuacha.

Kikwete alikuwa miongoni mwa viongozi mbalimbali wa Serikali na kisiasa waliofika kutoa salamu za pole kwa ndugu, jamaa na marafiki nyumbani kwa Mengi, Kinondoni jijini Dar es Salaam, jana.

Mengi aliyezaliwa Mei 29, 1942 mkoani Kilimanjaro, alifikwa na mauti Mei 2 akiwa Dubai, Falme za Kiarabu ambapo mwili wake unatarajia kuwasili kesho nchini.

Baada ya kuwasili saa 8 mchana utapelekwa Hospitali ya Jeshi Lugalo ambapo keshokutwa utaagwa katika viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam kisha utapelekwa nyumbani kwake na Jumatano asubuhi utasafirishwa kwenda Machame, Kilimanjaro kwa ajili ya mazishi yanayotarajiwa kufanyika Alhamisi kijijini kwao, Nkuu - Machame.

Akitumia chini ya dakika saba kutoa salamu zake, Kikwete aliyekuwa Rais wa awamu ya nne, alisema Mengi alikuwa ni mtu mwenye huruma na moyo wa kuwasaidia watu mbalimbali, na ametumia utajiri wake kuwasaidia Watanzania wengi.

Alisema Taifa lilitamani kuendelea kuwa na mfanyabiashara huyo, lakini Mungu ameshapitisha uamuzi wake na kilichobaki ni familia kuwa na moyo wa subira.

“Tuendelee kuwa watulivu, tuache uongo, tuache kuingiza yasiyokuwepo na kuichanganya jamii, hiyo ndiyo kama kweli tunampenda Mengi haya yote tuache kutunga uongo,” alisema.

“Tusubiri ukweli, amefariki Dubai mdogo wake akiwepo, binti yake akiwepo, hawa ndio wana ukweli. Mengine mnayosema tuyaache, wakirudi wale watatuambia nini hasa, ilikuwaje mpaka kifo kikatokea, mimi ombi langu ni hilo.”

Akizungumza kwa sauti ya utulivu, Kikwete alisema, “nilishtushwa na taarifa za kifo chake, si rahisi kuzungumza kutokana na hali ya majonzi.Nilikuwa Benin katika mkutano wenye ajenda ya kutokomeza malaria ndipo nilipopata taarifa hizi.”

“Kabla ya umauti kumkuta nilizungumza na kusalimiana naye kwa sababu alikuwa kama kaka yangu. Nilikubaliana naye kwamba nikirudi safari tutakutana na kuzungumza, kifo chake kimenishtua sana.”

Alisema, “nimezungumza na mtoto wa Mengi aitwaye Abdiel nikamwambia ‘Mengi ameishi yake na amefanya mambo mengi. Basi yale aliyoyafanya yadumishwe na watoto ili bendera ya IPP iendelee kupepea.”

Pia, Kikwete alisema ni wakati wa Watanzania kuwaombea watoto na familia ya Mengi ili wayasimamie kwa ufanisi yale yaliyoachwa.

Kijijini Nkuu

Jana, waombolezaji waliendelea kujitokeza kutoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wa familia hiyo katika kijiji cha Nkuu, Machame mkoani Kilimanjaro.

Mkuu wa kituo cha polisi Wilaya ya Hai, Lwelwe Lukandampina akizungumza nyumbani hapo alisema wamejipanga kuimarisha ulinzi kuanzia Uwanja wa Ndege Kilimanjaro (KIA) mpaka kijijini hapo siku mwili utakapofikishwa.

Imeandikwa na Fortune Francis, Bakari Kiango (Dar) na Janeth Joseph (Moshi)