Kila kukicha CUF afadhali ya jana

Muktasari:

  • Mlolongo wa matukio ya kushangaza yanayosababishwa na pande mbili za kiuongozi zinazovutana umekifanya chama hicho kutotekeleza majukumu yake ipasavyo, hata hivyo mara hii upande mmoja umekuja na jipya

Dar es Salaam. Kuna msemo maarufu wa Kiswahili usemao “kila kukicha ni afadhali ya jana”. Huu unasadifu migogoro inayoibuka ndani ya CUF.

Mwaka mmoja baada ya Uchaguzi Mkuu, chama hicho kimekuwa katika mgogoro wa uongozi baada ya Profesa Ibrahim Lipumba kufuta barua yake ya kujiuzulu uenyekiti aliyoiandika mwaka 2015 na katibu wake mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad akaongoza wanachama waliopinga kurejea kwake madarakani.

Lipumba alikuwa akipinga CUF kuwa katika Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ulioazimia kumsimamisha Edward Lowassa kuwa mgombea urais pekee wa upinzani, akisema “dhamira inamshtaki”.

Tangu hapo, Maalim Seif na Profesa Lipumba, ambaye alitambuliwa na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, hawajawahi kuketi meza moja, kila upande ukiongoza kundi lake.

Mgogoro huo ulifika mahakamani ambako pande zote zinasubiri hukumu.

Lakini katika uamuzi mdogo, Februari 21, Mahakama Kuu ilitengua uteuzi wa wajumbe wa bodi ya wadhamini wa kambi ya Profesa Lipumba na kutoyatambua majina ya wajumbe yaliyopendekezwa na kambi ya Maalim Seif kwa sababu hawakuwa na sifa.

Uamuzi huo umeibua mapya. Profesa Lipumba ametangaza majina mapya ya wajumbe, kazi ambayo pia imefanywa na kambi ya Maalim Seif.

Wakati Mahakama Kuu ikitarajiwa kutoa hukumu kuhusu uhalali wa uenyekiti wa Profesa Lipumba, jana CUF upande wa mwenyekiti huyo ulitangaza kuitisha uchaguzi mkuu utakaofanyika Machi 14 – 15, ukitanguliwa na mkutano mkuu maalumu utakaofanyika Machi 12 kwa ajili ya ajenda moja ya mabadiliko ya katiba ya CUF.

Alipoulizwa jana kuhusu mkutano huo, Maalim Seif alisema “ikiwa ametangaza mkutano mkuu na tarehe zake ina maana haheshimu maamuzi ya mahakama. Kwa maoni yangu hatafanikiwa, kwani ni challenge (changamoto) kwa mahakama”.

Akitangaza uchaguzi huo jana jijini Dar es Salaam, kaimu naibu katibu mkuu wa CUF, Mneke Jafar aliwataka wanachama wenye sifa za kugombea nafasi yoyote ndani ya chama kuchukua fomu na kwamba mwisho wa kuzirejesha ni Machi 8.

“Mtu yeyote anayedhani anafaa kuwa mwenyekiti wa taifa, makamu mwenyekiti au katibu mkuu, milango iko wazi. Aje achukue fomu na ifikapo Machi 8, itakuwa siku ya mwisho kurudisha fomu hizo,” alisema.

Mbali na uchaguzi, alisema CUF itafanya mabadiliko ya katiba kwa lengo la kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na sheria mpya ya Huduma za Vyombo vya Habari.

Mneke alisema Oktoba 18 mwaka jana, walipokea barua kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ikivitaka vyama kubadili katiba zao ili kuruhusu viongozi kujiuzulu baada ya mkutano mkuu kufanyika.

“Sababu nyingine ya kubadilisha katiba yetu ni kutekeleza sheria mpya,” alisema.

“Sisi ni miongoni mwa vyama ambavyo tuliipinga sana hii sheria, lakini ndiyo imeshapitishwa. Hatuna namna, lazima twende nayo sawa.”