Kilichojiri kesi ya Mpemba aliyetajwa na Magufuli hiki hapa

Muktasari:

  • Kesi inayomkabili Yusuf Ali maarufu Mpemba wa aliyetajwa na Magufuli ya uhujumu uchumi imeendelea leo Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam

Dar es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi, inayomkabili Yusuf Ali au Mpemba aliyetajwa na Rais Magufuli na wenzake watano, umedai upo katika hatua za mwisho za uandaaji wa nyaraka kabla ya kuipeleka katika hatua nyingine.

Yusuph na wenzake watano wanakabiliwa na mashtaka manne, likiwemo la kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh785.6milioni.

Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi akisaidiana na Elizabeth Mkunde, amedai hayo, leo Jumatano Oktoba 24, 2018 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo,  Thomas Simba wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

Nchimbi amedai wapo katika hatua za mwisho za uandaaji wa nyaraka kwa ajili ya kuipeleka kesi hiyo katika hatua nyingine, hivyo wanaomba ahirisho la mwisho ili waweze kukamilisha.

Baada ya Nchimbi kueleza hayo, wakili wa utetezi, Nehemia Nkoko aliutaka upande wa mashtaka kukamilisha shughuli hiyo kwa haraka ili kesi iweze kuendelea na hatua nyingine.

Hakimu Simba baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote,  ameahirisha kesi hiyo hadi Novemba 6, 2018 kesi hiyo itakapotajwa.

Mbali na Yusuph, washtakiwa wengine katika kesi hiyo  ni Charles Mrutu, mkazi wa Mlimba, Morogoro, Benedict Kungwa, mkazi wa Mbagala Chamazi, Jumanne Chima, mkazi wa Mbezi, Ahmed Nyagongo, dereva na Pius Kulagwa.

Washtakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka manne ya kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh785.6milioni.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, katika tarehe tofauti kati ya Januari, 2014 na Oktoba, 2016 wakiwa Dar es Salaam, Tanga, Iringa na Mtwara, walijihusisha na mtandao wa ujangili kwa kukusanya na kuuza nyara za Serikali ambazo ni vipande 50 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Dola za Marekani 180,000 sawa na Sh392.8milioni bila kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Katika mashitaka ya pili inadaiwa, Oktoba 26, 2016 wakiwa Mbagala Zakhem, walikutwa na vipande 10 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilo 13.85 vikiwa na thamani ya dola za Marekani 30,000  (Sh 65.4milioni ).

Oktoba 27, 2016, wakiwa Tabata Kisukuru walikutwa na vipande vinne vya meno hayo vyenye uzito wa kilo 11.1 vikiwa na thamani ya dola za Marekani 15,000 (Sh32.7 milioni).

Pia, Oktoba 29, 2016 walikutwa na vipande 36 vyenye thamani ya Sh 294.6 milioni bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.