Kilio cha wakulima chamchosha Majaliwa, atoa agizo Wizara ya Kilimo

Muktasari:

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imechoshwa kusikia kilio cha wakulima kuhusu mbegu zisizokuwa na ubora na viuatilifu hafifu ataka Wizara ya Kilimo kumaliza tatizo


Mwanza. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali imechoka kusikia vilio vya wakulima hususani wa pamba wakilalamikia ubora wa mbegu na viuatilifu.

Kutokana na hali hiyo ameiagiza Wizara ya Kilimo kuhakikisha inasimamia na kuondoa kasoro zote zinazojitokeza na kuibua kero kwa wakulima.

Ametoa kauli hiyo leo Machi 19, 2019 wakati akizindua rasmi Benki ya Maendeleo ya Kilimo kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa jijini Mwanza.

"Benki hii imepiga hatua lakini changamoto kubwa imebaki kwa mbegu, tena leo nataka nijue hizi mbegu na mbegu manyoya ndio nini maana wakulima kila mwaka wanapiga kelele na ubovu wa mbegu.”

“Tumechoka kusikia malalamiko haya wakati kuna chuo cha utafiti wa mbegu cha Ukirigulu, mnashindwa nini kumaliza tatizo hili, waziri peleka salamu wizarani," amesema Majaliwa.

Amesema kila mwaka wanajiwekea malengo ya kilimo cha pamba lakini hayafikiwi na watendaji hawajiulizi kupata ufumbuzi wa changamoto hizo.

"Mbinu duni za uzalishaji kila mwaka tunaweka malengo lakini hatuyafikii, hili hatutaki kuona likijitokeza kwa miaka ijayo maana tumewaacha wakulima wakiteseka wenyewe kila mmoja analima anavyojua," amesema.

Amesema Wizara ya Kilimo ndiyo yenye wataalamu wengi lakini ndiyo inayoongoza kwa changamoto na lawama kutoka kwa wakulima.

Pia amewaagiza wakuu wa mikoa yote kuwasimamia maofisa kilimo kuondoka maofisini kwenda maeneo ya wakulima ili kuwaelekeza jinsi ya kulima kilimo cha tija.

Amesema Serikali inataka kuwapo na viwanda vingi vya kuchakata mazao ili kuwaondolea adha wakulima.

Amesema Serikali inatumia fedha nyingi kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi hivyo wanataka kuondoa hali hiyo.

Majaliwa ameziagiza benki zote nchini kukaa kuangalia upya na kujitathmini riba wanazotoza kwa wateja akidai ni kubwa NA hazilengi kuwanufaisha watu wa hali ya chini.

"Nenda mpunguze riba zenu, wananchi wengi wanaogopa kuzisogelea benki wanaziona kama kituo cha polisi, Serikali tusingependa kuona hilo likiendelea, lazima tuwawezeshe wakulima ili waone kama kilimo ni kimbilio kwao,” amesema.

Pia amewataka wakulima kujitokeza kwa wingi kwenda kukopa katika benki hiyo maana imeanzishwa kwa ajili yao.

Naye Naibu Waziri wa Kilimo, Innocent Bashungwa ameiagiza benki hiyo kuanzisha kitengo maalumu cha kuwaelekeza wakopaji katika benki hiyo jinsi ya kuandika maandiko ya kitaalamu ili waweze kukopeshwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Japhet Justin amesema hadi kufikia Februari 2019 benki hiyo imefikisha mtaji wa Sh68 bilioni na kwamba kiasi hicho ni sawa na ongezeko la asilimia 13 ya Sh60 bilioni walizopewa na Serikali mwaka 2015 benki hiyo ilipoanza kufanya kazi rasmi.

"Mpaka sasa tumeshatoa mikopo yenye thamani ya Sh107 bilioni na kati ya fedha hiyo tayari imesharejeshwa Sh31.4 bilioni ," amesema Justin.

Amesema kwa upande wa kilimo cha pamba kwa mwaka 2018, benki hiyo ilitumia Sh6.6 bilioni kwa ajili ya kununua pembejeo na viuatilifu kwa wakulima zaidi ya 200,000.

"Upande wa kahawa tulitumia Sh30 bilioni na kwa sasa kuna ekari zaidi ya 2,000 wilayani Buchoswa ambazo zimetengewa zaidi ya Sh2 bilioni.’’ Amesema.

Kuhusu alizeti amesema wametenga Sh800 milioni kujenga kiwanda cha alizeti wilayani Kahama mkoani Shinyanga na katika ufugaji, benki inatarajia kufungua kiwanda ambacho kitakuwa na uwezo wa kuchinja ng'ombe 125 ambapo wametenga Sh8 bilioni kwa ajili ya kiwanda hicho.

Amesema katika sekta ya uvuvi pia wametenga Sh40 bilioni ambazo zitakopeshwa katika sekta hiyo ili kujenga viwanda vya kuchakata samaki.

Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa benki hiyo, Rosebert Kulwijila amesema tangu benki hiyo ianzishwe wameshakopesha matrekta 50 kwa wakulima katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Amesema jumla ya wakulima 6,864 watanufaika na matrekta hayo yanayoendelea kutolewa na benki hiyo ambapo kwa leo pia Waziri Mkuu aanatarajiwa kukabidhi matrekta 16 kwa viongozi wa vyama vya ushirika.

Mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella amesema mkoa una benki 28 za kibiashara zenye matawi 26 kwenye halmashauri zote za mkoa huo sawa na zaidi ya asilimia 90 ya benki zote.