Kimbunga Keneth chatua Comoro

Muktasari:

Kimbunga hicho sasa hivi kinaelekea Msumbiji katika jimbo la Cabo Delgado

Harare,Zimbabwe.Taarifa ya wizara ya habari Zimbabwe imeeleza kwamba, Kimbunga Kenneth kinachotarajiwa kuzikumba nchi za Msumbiji, Malawi na baadhi ya maeneo ya Zimbabawe kimeingia visiwa vya Comoro.

Kimbunga hicho kimefika daraja la nne kikiambatana na upepo wa kasi ya 130 mph karibu na eneo la kati na kinaarifiwa kuelekea Msumbiji katika jimbo la Cabo Delgado.

Wataalamu wa hali ya hewa wanaonya kuwa kimbunga Kenneth kinatazamiwa kuwa na nguvu sawa na kimbunga Idai ambacho kilizikumba nchi tatu Msumbiji, Zimbabwe na Malawi mwezi uliopita na kusababisha maafa makubwa.

Taarifa kutoka Zimbabwe zinasema kwamba kutokana na uzoefu wa athari ya kimbunga Idai mwezi uliopita, watu wote wanaoishi katika maeneo hatarishi kama Mbire Muzarabani na maeneo ya chini ya jimbo la Masvingo na kwingineko wanatakiwa kujihadhari mapema.