Kimbunga idai kilichoua watu nchi tatu chatoa somo nchini

Nchi za Afrika Mashariki hususan Kenya na Tanzania zitaathiriwa na kimbunga Idai kilichozikumba Msumbiji, Zimbabwe na Malawi na kusababisha vifo.

Watu takriban 1,000 wanakadiriwa kufariki dunia kutokana na kimbunga hicho nchini Msumbiji wakati Malawi na Zimbabwe nako zaidi ya watu 100 wamethibitika kupoteza maisha kwa mujibu wa mamlaka za Serikali.

Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji anasema hilo ni janga la kibinadamu nchini mwake.

Meneja wa Kituo Kikuu cha Utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Samwel Mbuya ameliambia Mwananchi kwamba tayari athari za kimbunga hicho kilichoharibu nyumba 20,000 Zimbabwe zimeonekana hapa nchini kutokana na upungufu wa mvua.

Anasema, “kwa sasa kimbunga Idai kimeshaangukia nchi kavu na katika kipindi cha kuwepo kwake katika rasi ya Msumbiji kwenye Bahari ya Hindi kimetusababishia upungufu wa mvua za masika hususan maeneo ya Kaskazini mwa nchi.”

“Nchi za Kusini mwa Afrika; Msumbiji, Malawi na Zimbabwe ndizo zimepata athari ya mvua nyingi na mafuriko.”

TMA yafafanua

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TMA ikielezea kwa undani tathmini ya mifumo ya hali ya hewa inaeleza kuwa katika kipindi hiki, migandamizo mikubwa ya hewa iliyopo Kaskazini mwa dunia (Azore na Siberia) inatarajiwa kuimarika wakati ile iliyopo kusini (St. Helena na Mascarene) inatarajiwa kudhoofika.

Imeeleza kuwa hali hiyo inasababisha kupungua kwa msukumo wa hewa angani - Kaskazini mwa Tanzania ambapo joto la bahari la chini ya wastani linatarajiwa kuendelea katika eneo la magharibi mwa Bahari ya Hindi hali inayotarajiwa kuzuia upepo kutoka Kaskazini-mashariki, hivyo kupunguza mvua katika maeneo hayo. Imefafanua kuwa maeneo ya Kusini-magharibi joto la bahari linatarajiwa kuwa juu ya wastani na kusababisha kutokea kwa vimbunga baharini.

Joto la bahari la wastani linatarajiwa katika eneo la Kusini-Mashariki mwa bahari ya Atlantiki (karibu na pwani ya Angola).

Hata hivyo, inasema hali hiyo haitarajiwi kusababisha mabadiliko makubwa ya mifumo ya hali ya hewa katika maeneo ya Magharibi mwa nchi.

Imeeleza hali ya joto la juu ya wastani kwa sasa katika maeneo ya Kusini-magharibi mwa bahari ya Hindi imesababisha kutokea kwa kimbunga Idai.

“Kimbunga hiki kimesababisha hali ya ukavu katika maeneo ya kaskazini mwa nchi,” inasema sehemu ya taarifa hiyo.

TMA imetoa angalizo kuwa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Kilimanjaro, Arusha na Manyara pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba kunatarajiwa kuendelea kuwapo kwa vipindi vya hali ya ukavu.

Taarifa ya TMA inashabihiana na ile iliyotolewa na maofisa wa kitengo cha utabiri wa hali ya hewa nchini Kenya wakionya kuwa athari ya kimbunga Idai itashuhudiwa katika baadhi ya maeneo ya Afrika Mashariki.

Naibu mkurugenzi wa idara ya utabiri wa hali ya hewa nchini humo, Benard Chanzu anasema kimbunga hicho huenda kikaathiri msimu wa mvua eneo hilo.

Kimbunga hicho kilichoanza kuvuma Alhamisi iliyopita nchini Msumbiji kinavuma kwa kasi ya kilomita 177 kwa saa huku mji uliopo kando ya bandari wa Beira katika Jimbo la Sofala nchini humo ukiwa uliloathirika zaidi na mafuriko.

Serikali ya Msumbiji inasema watu 84 wamethibitika kufariki dunia na wengine 100,000 wanahitaji kuokolewa kwa dharura karibu na mji huo.

Shirika la Msalaba Mwekundu linasema takriban watu 400,000 hawana makazi nchini humo.

Hali ilivyo

Mamia ya watu bado hawajaokolewa kutoka katika maeneo waliyokwama kutokana na miundombinu ya barabara kusombwa na maji hivyo kusababisha ugumu kufikiwa.

Clare Nullis, ofisa wa taasisi ya hali ya hewa ya Umoja wa Mataifa (UN), anasema hilo ni moja ya majanga makubwa kuwahi kuukumba upande wa Kusini mwa Afrika.

Mashuhuda wanasema kimbunga hicho kilianza kuvuma kama upepo wa kawaida, lakini baadaye kiliongezeka na kuanza kuezua mapaa, kung’oa miti na kuharibu miundombinu mjini Beira.

“Siku hiyo tulikuwa na sherehe ya kuzaliwa kwa mtoto wetu, hivyo sote nyumbani tulirejea mapema, baadaye tukaanza kuona watu wakikimbia huku na kule mitaani kutokana na upepo ulioambatana na mvua,” anasema Nelson Moda, mkazi wa Beira.

Picha za juu zilizopigwa katika eneo hilo zinaonyesha karibu kilomita 50 ya eneo la nchi kavu lilikuwa limemezwa na maji baada ya mto Buzi kuvunjika kingo zake na kusababisha mafuriko, linaeleza shirika la kimataifa la misaada la Save the Children.

Tayari vikosi vya uokoaji vinaendelea na shughuli za uokozi kuwanusuru waliokwama kwenye mapaa ya nyumba zilizozingirwa na maji, juu ya miti na kwingineko walikojihifadhi kuokoa maisha yao.

Nchini Zimbabwe, Serikali inasema watu 98 wamefariki dunia kutokana na kimbunga hicho na wengine zaidi ya 200 hawajulikani walipo.

Rais Emerson Mnangagwa anasema Serikali yake inaendelea kutoa misaada kwa walioathirika na maafa hayo.

Miongoni mwa maeneo yaliyoathiriwa zaidi na janga hilo ni mji wa Chimanimani uliopo Kusini-mashariki mwa Zimbabwe.

Mafuriko pia yamezikumba baadhi ya sehemu za Malawi ambako zaidi ya watu 50 wameripotiwa kupoteza maisha na wengine kukosa makazi, na kulazimika kuhifadhiwa katika kambi maalumu zilizotengwa na Serikali.

Hata hivyo, Kanali Matamwe Said, mkurugenzi wa Idara ya maafa katika Ofisi ya Waziri Mkuu hapa nchini, anasema kuwa walishachukua tahadhari kuhusiana na kimbunga hicho. “Tulichukua tahadhari kufuatia utabiri wa hali ya hewa uliotolewa mapema kabla ya kimbunga hicho na baada kutokea,” anasema.

Anasema kuwa kutokana na taarifa za uwezekano wa kuwapo kwa kimbunga hicho, wameandika barua kwenda Ofisi ya Rais (Tamisemi) kuwataarifu wakuu wa mikoa kuchukua tahadhari ili kuepuka maafa kama yaliyotokea kwenye nchi hizo na mvua za vuli zinazonyesha kwenye baadhi ya mikoa nchini.

Jinsi vimbunga vinavyopewa majina

Kwa mujibu wa BBC, vimbunga katika maeneo ya bahari ya Atlantiki, Caribbean na Ghuba ya Mexico hupewa majina ya Shirika la Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani (WMO) ambalo lina makao yake makuu nchini Uswisi.

Linasema zamani ni majina ya kike pekee ndiyo yaliyotumiwa, lakini kuanzia 1979 majina ya kiume yalianza kutumika.

Huwa kuna makundi sita ya majina ambayo hutumiwa kwa mzunguko.

Hii ina maana kwamba majina yaliyotumiwa kwenye vimbunga mwaka 2016 hayatatumiwa tena hadi 2022.

Hata hivyo, baadhi ya majina huacha kutumika kunapotokea uharibifu au hasara kubwa kwani kutumia tena kutafufua kumbukumbu zenye uchungu.

Mfano ni kimbunga Katrina kilichoua watu 2,000 mwaka 2005 na kusababisha uharibifu mkubwa Marekani.

Kimbunga hicho kilisababisha watu milioni moja kupoteza makazi huku miji ya New Orleans na Louisiana ikiathirika zaidi.

Inasema katika maeneo mengine majina hupatikana kwa kundi la wataalamu la WMO liitwalo Kamati ya Vimbunga vya Tropiki ambalo hukutana kila mwaka.

Kundi hilo ndilo huamua ni majina yapi yatatumika tena na ni yapi yataacha kutumiwa. Majina yaliyoacha kutumiwa mbali na Katrina, ni Mitch, kutokana na kimbunga cha mwaka 1998 kilichoua watu 11,000 Honduras na Nicaragua. Kimbunga hicho ndicho kibaya zaidi kuyakumba maeneo ya Magharibi mwa dunia katika kipindi cha miongo miwili iliyopita.